Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi, leo tarehe 24 Agosti 2026, amezindua na kuongoza hafla ya ugawaji wa pampu 113 za umwagiliaji kwa wakulima wadogo wa Mkoa wa Mara, iliyofanyika katika viunga vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara. Hafla hiyo imeandaliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Kanali Mtambi amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Mara, hususan wakulima, kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Serikali kwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa wananchi.
Aidha, amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuupa kipaumbele Mkoa wa Mara kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo, afya, elimu, miundombinu na huduma za kijamii ikiwa ni utekelezaji wa Dira ifikapo mwaka 2050. Pia ameishukuru Wizara ya Kilimo pamoja na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa juhudi zao za kuendeleza sekta ya umwagiliaji na kuwawezesha wakulima kupata teknolojia na vifaa vinavyoongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Mheshimiwa Mtambi amesema maendeleo ya sekta ya kilimo yanategemea matumizi ya sayansi na teknolojia, hivyo amewataka maafisa ugani kuendelea kuwapatia wakulima elimu ya matumizi ya mbegu bora, mbinu za kisasa za kilimo, taarifa za hali ya hewa pamoja na ushauri wa kitaalamu ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Mara, Adeliaidy Rutashobya, amesema mkoa una jumla ya vikundi 80 vya umwagiliaji vinavyowahusisha wakulima 121.
Ameeleza kuwa ugawaji wa pampu 113 za umwagiliaji utasaidia kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji, kuimarisha uzalishaji wa mazao na kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha uhakika katika misimu yote ya mwaka.
Wakulima walionufaika na mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia pampu hizo, wakieleza kuwa zitasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, kuboresha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha kaya zao pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Mara.










Comments
Post a Comment