MASABALA MZEE MASHUHURI KAGERA ATUNUKIWA TUZO BAADA YA KUTOA ARDHI KWA AJILI YA BWENI LA WANAFUNZI-KIBETA
Na Angela Sebastian
Mzee mashuhuri wa Mkoa wa Kagera, Joseph Masabala, amepewa hati ya shukrani na tuzo maalum baada ya kutoa sehemu ya ardhi yake kwa ajili ya ujenzi wa Bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kibeta, Manispaa ya Bukoba, hatua inayotajwa kuwa mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wa eneo hilo.
Tuzo hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea na kuzindua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba. Mzee Masabala pamoja na mkewe, Lushaka Masabala, walipokea hati hiyo ya shukrani na tuzo kwa niaba ya familia yao.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwang’onda ameipongeza familia ya Mzee Masabala kwa uamuzi wao wa pamoja wa kutoa ardhi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya elimu, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano wa uzalendo na kujitolea kwa jamii. Amesema ardhi hiyo haitakuwa tu sehemu ya ujenzi wa mabweni, bali itakuwa mkombozi wa elimu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mwang’onda amesema mchango wa familia hiyo unaonesha umuhimu wa wananchi kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi, hususan upatikanaji wa miundombinu bora ya elimu. Ameeleza kuwa uwepo wa mabweni utasaidia wanafunzi kupata mazingira rafiki ya kusoma na kuongeza muda wa kujifunza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amesema ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari Kibeta utasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo usafiri na umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi hadi shuleni.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilipotembelea Shule ya Sekondari Kibeta, pia zilizindua vyumba viwili vya madarasa pamoja na kukabidhi madawati kwa wanafunzi. Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali na wananchi katika kuboresha miundombinu ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Kwa ujumla, Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Manispaa ya Bukoba umezindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 900. Mchango wa Mzee Joseph Masabala na familia yake umeongeza uzito wa ziara hiyo, ukitoa funzo kuwa nguvu ya pamoja kati ya Serikali na wananchi inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii.




Comments
Post a Comment