Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara, ameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kutenga maeneo yanayodaiwa kuwa na madini katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Serengeti, ili kuwawezesha vijana wa maeneo hayo kushiriki katika shughuli za uchimbaji na kunufaika kiuchumi.
Waitara ametoa ombi hilo leo, Agosti 26, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, akitaka kujua ni lini Serikali itachukua hatua kuhusu maeneo hayo na kuwawezesha vijana kupata fursa za uchimbaji.
Mbunge huyo amesema taarifa za kuwepo kwa madini katika maeneo hayo zimeibua matarajio kwa wananchi, hususan vijana, ambao wanahitaji fursa za ajira na shughuli za kuwawezesha kujipatia kipato.
Akijibu swali hilo, Dkt. Kiruswa amesema Serikali ina utaratibu wa kisheria wa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini, ikiwemo maeneo yenye matumizi mengine maalumu, endapo taratibu zote zinazotakiwa zitazingatiwa.
Amesema matumizi ya maeneo nchini yanaongozwa na sheria mbalimbali, hivyo maeneo ya hifadhi, malisho na maeneo mengine yenye matumizi maalumu hayawezi kutumika kwa shughuli za uchimbaji bila kufuata taratibu zilizowekwa.
“Kwa mujibu wa sheria zetu na matumizi ya maeneo mbalimbali yaliyotengwa nchini, kuna utaratibu wa kuweza kuyatenga maeneo hayo kwa ajili ya wachimbaji wanaokuwa tayari kuwekeza,” amesema Dkt. Kiruswa.
Naibu Waziri huyo ametoa mfano wa madini ya urani katika eneo la Mto Mkuu, akisema eneo hilo awali lilikuwa sehemu ya eneo la akiba, lakini baadaye lilitengwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji baada ya taratibu za kisheria kufuatwa.
Amesema mfano huo unaonesha kuwa pale ambapo kuna rasilimali kubwa za madini, uwezekano wa eneo kutengwa kwa ajili ya uchimbaji unaweza kuwepo, mradi taratibu za kisheria na matumizi ya ardhi zizingatiwe.
Kwa mantiki hiyo, Dkt. Kiruswa amesema suala la maeneo yenye madini katika eneo la Serengeti linaweza kufanyiwa kazi iwapo taratibu zinazotakiwa kisheria zitafuatwa, hatua ambayo inaweza kufungua fursa kwa wachimbaji na wananchi kunufaika na rasilimali zilizopo.
Waitara amesisitiza umuhimu wa Serikali kuangalia suala hilo kwa uzito, akieleza kuwa kufunguliwa kwa fursa hizo kutasaidia kuongeza ajira na shughuli za kiuchumi kwa vijana wa Tarime na maeneo jirani


Comments
Post a Comment