RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Makamu wa Rais, Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, kutambua kuwa cheo alichokabidhiwa si ufalme bali ni dhamana ya kuwatumikia Watanzania kwa uzalendo, uadilifu, bidii na uwajibikaji.
Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo, Agosti 29, 2026, katika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, wakati akizungumza katika hafla ya kumuapisha Mheshimiwa Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Cheo si ufalme, ni dhamana. Dhamana uliyopewa ni ya kuwatumikia Watanzania,” amesema Rais Dkt. Samia.
Amesema nafasi ya Makamu wa Rais inahitaji kiongozi mwenye uwezo wa kuwaunganisha wananchi, kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali na kuhakikisha maslahi ya Taifa yanapewa kipaumbele katika kila hatua.
Rais Dkt. Samia amesema uzoefu wa Mheshimiwa Ndejembi katika nafasi mbalimbali za uongozi alizowahi kushika Serikalini, pamoja na uwezo wake wa kujifunza, kufuatilia na kusimamia majukumu aliyopewa, ni msingi mzuri wa kumwezesha kutekeleza majukumu yake mapya.
Ametoa rai kwa Makamu wa Rais kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano, ushirikiano na utulivu nchini, huku akishirikiana kwa karibu na viongozi wengine katika kuhakikisha shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa ufanisi.
“Uongozi ni kutumikia watu, hivyo dhamana hii itumike kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema matarajio ya wananchi kuhusu maendeleo yanaweza kutimia iwapo viongozi na Serikali wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu, uwajibikaji na kuzingatia misingi ya uongozi bora.
Amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji viongozi wenye uwezo wa kusukuma utekelezaji na kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameipongeza Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa kuridhia jina la Mheshimiwa Ndejembi, akisema mchakato huo ulizingatia uwezo, uzoefu na sifa zake za kiuongozi.
Amesema umri wa Mheshimiwa Ndejembi unampa fursa ya kutumia nguvu, maarifa na uzoefu alionao katika kulitumikia Taifa, huku akimtaka kuendelea kujifunza na kukua katika majukumu yake mapya.
Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi na uteuzi wake kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.





Comments
Post a Comment