Na Angela Sebastian; Bukoba
Mwenge wa Uhuru Kuzindua na Kukagua Miradi 54 ya Sh. Bilioni 23 Kagera
Mwenge wa Uhuru mwaka huu unatarajiwa kuzindua, kufungua, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 54 ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni 23 mkoani Kagera.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 26, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, amesema Mwenge huo utapokelewa wilayani Muleba ukitokea mkoani Geita tarehe Agosti 30, 2026, kabla ya kuanza kukimbizwa katika halmashauri nane za mkoa huo.
Kwa mujibu wa Kanali Kido, Mwenge wa Uhuru utatembea umbali wa takribani kilomita 1,230 ndani ya Kagera, huku ukiifikia miradi 54 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo,katika miradi hiyo, 25 itawekewa mawe ya msingi, mitano itafunguliwa, 11 itazinduliwa na 13 itakaguliwa ili kujiridhisha na utekelezaji wake pamoja na manufaa yake kwa wananchi.
Miradi hiyo inahusisha sekta muhimu za maendeleo, ikiwemo maji, afya, elimu, miundombinu, nishati, uwezeshaji wa vijana kiuchumi, pamoja na mazingira wezeshi kwa uwekezaji.
Kanali Kido amesema ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu unalenga kuendelea kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia kaulimbiu:
“Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”
Amesema Mwenge huo pia utatumika kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, malaria, VVU/UKIMWI na dawa za kulevya, sambamba na kuhimiza wananchi kuzingatia lishe bora.
Aidha mkuu huyo wa mkoa amewaalika wananchi wote wa Kagera kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru katika maeneo mbalimbali utakakopita, akisisitiza umuhimu wa kuonyesha mshikamano na kuunga mkono jitihada za maendeleo.
“Niwaalike wananchi wote kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru mkoani Kagera. Tuupokee kwa bashasha na shangwe utakapowasili katika maeneo yetu ili kuonyesha ishara ya umoja, amani na mshikamano sisi wana Kagera,” amesema Kanali Kido.
Aidha, amewataka wananchi kujitokeza katika maeneo ya mapokezi, kando ya barabara, kwenye miradi itakayofikiwa na Mwenge pamoja na maeneo ya mikesha katika wilaya zote.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukamilisha mbio zake mkoani Kagera Septemba 6, 2026, kabla ya kukabidhiwa kwa mkoa wa Kigoma Septemba 7, 2026.



Comments
Post a Comment