MBUNGE wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, ameitaka Serikali kueleza hatua inazochukua kuhakikisha wananchi wa vitongoji 109 katika jimbo hilo vinapatiwa huduma ya umeme.
Akizungumza leo, Agosti 26, 2026, wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Mahera amesema wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu huduma hiyo na kutaka kujua lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme.
Akijibu, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya usambazaji umeme nchini kwa kuzingatia ahadi za Serikali, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema fedha zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, huku akieleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa na huduma ya umeme yanaunganishwa kabla ya mwaka 2030.
Naibu Waziri Makamba amempongeza Dkt. Mahera kwa kufuatilia maendeleo ya jimbo lake na kumtaka kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili wananchi wa Butiama wanufaike na huduma ya umeme.


Comments
Post a Comment