Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania wanatarajiwa kunufaika na huduma za afya bure, ukarabati wa vituo vya afya pamoja na misaada ya kijamii kupitia Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoendeshwa na majeshi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Wiki hiyo imezinduliwa leo jijini Dar es Salaam na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kijeshi katika kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika viwanja vya Golf Lugalo, Luteni Jenerali Othman amesema ushirikiano wa majeshi ya EAC si suala la ulinzi na usalama pekee, bali pia ni nyenzo ya kuimarisha mshikamano na ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki.
Amesema kuandaliwa kwa shughuli hizo nchini Tanzania kwa mara ya pili ni ishara ya imani na uaminifu uliopo kwa Tanzania na JWTZ katika kuendeleza ushirikiano wa kikanda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sita ya Ushirikiano wa Majeshi ya Afrika Mashariki 2026, Brigedia Jenerali JWTZ Dkt. Agatha Mary Katua, amesema shughuli hizo zimeandaliwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya majeshi na wananchi.
Amesema wananchi watapata huduma mbalimbali zikiwemo huduma za afya bure, ukarabati wa vituo vya afya na misaada ya kibinadamu kwa makundi yenye mahitaji maalumu.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Katua, vikosi kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Somalia na Uganda vitashiriki katika shughuli hizo zitakazofanyika Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Pemba na Unguja, pamoja na maeneo mengine yatakayofikiwa na timu maalumu.
Ameeleza kuwa huduma za afya zitatolewa katika hospitali na vituo vilivyochaguliwa, huku shughuli nyingine zikihusisha ukarabati wa vituo vya afya na utoaji wa misaada kwa vituo vya watoto yatima, magereza na vituo vya watu wenye mahitaji maalumu.
Shughuli hizo zitafanyika kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 1, 2026, ambapo hafla ya kufunga itaambatana na maadhimisho ya miaka 62 ya JWTZ tangu kuanzishwa kwake Septemba 1, 1964.





Comments
Post a Comment