Mhe. Bulaya ametoa ombi hilo leo, Agosti 26, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu–TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe.
Akizungumzia changamoto ya nyumba za walimu, Mhe. Bulaya amesema baadhi ya halmashauri zimeanza ujenzi wa nyumba hizo lakini zinakabiliwa na ukosefu wa fedha za kukamilisha miradi hiyo, hivyo kuiomba Serikali kuhakikisha inazipatia fedha ili kukamilisha majengo hayo.
Pia ameitaka Serikali kuangalia changamoto ya mabweni katika shule mbalimbali, akitolea mfano baadhi ya shule zilizopo katika maeneo yenye umbali mkubwa na makazi ya wanafunzi, hali inayoweza kuwalazimisha wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata elimu.
Akijibu, Prof. Shemdoe amesema Serikali inatambua kuwa halmashauri nyingi zina uwezo mdogo wa mapato, ndiyo maana imeziweka katika makundi tofauti kulingana na uwezo wa mapato na mahitaji ya maendeleo.
Amesema baadhi ya halmashauri zinatakiwa kutenga asilimia 70 ya mapato kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku nyingine zikitenga asilimia 40 au 20, kulingana na kundi ililopo.
Prof. Shemdoe ameeleza kuwa Serikali tayari imepeleka Sh milioni 60 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu, huku ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha nyumba na miundombinu mingine iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Kuhusu ujenzi wa mabweni, Prof. Shemdoe amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwapo kwa mabweni katika shule zilizo mbali na makazi ya wananchi, kwa kuwa yanasaidia kuwaweka wanafunzi karibu na shule na kuongeza usalama wao.
“Serikali itaendelea kutafuta fedha ili tuone namna ya kujenga mabweni, hasa kwenye zile shule ambazo ziko mbali na makazi ya wananchi,” alisema Prof. Shemdoe.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita iko tayari kuendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga mabweni katika shule zenye uhitaji, ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu katika mazingira salama na rafiki.


Comments
Post a Comment