Mkurugenzi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Fredrick Salukele amesema ushiriki Tanzania katika mashindano ya ujuzi ya WorldSkills umefungua fursa mpya za kimataifa kwa vijana wenye ujuzi, huku tayari washiriki wawili wakikubaliwa kwenda Shanghai, China kama waangalizi wa Mashindano ya WorldSkills International 2026.
Akizungumza wakati wa Mashindano hayo yanayoendelea jijini Tanga, Selukele amesema vijana hao wanatoka katika fani za mtandao wa vitu na urembo tiba, hatua inayoonesha kuwa ujuzi wa Tanzania umeanza kutambulika kimataifa.
"Baada ya matokeo ya mashindano ya kitaifa kutangazwa, Tanzania itawasilisha washindi kwa WorldSkills ili kuitangazia dunia kuwa nchi yetu ina taasisi zinazozalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi viwango vya kimataifa,"amesema.
Amesema kuonekana katika majukwaa ya WorldSkills kunawaongezea vijana nafasi za ajira za kimataifa, huku Serikali ikilenga kuanzisha mfumo wa vyeti vinavyotambulika kimataifa ili kurahisisha wataalamu kufanya kazi katika nchi mbalimbali.
"Mfumo wa sifa za elimu ya ufundi wa Afrika Mashariki na SADC tayari umewekewa msingi wa kurahisisha uhamaji wa wanafunzi na wataalamu kati ya nchi wanachama kulingana na kiwango cha ujuzi walichopata,"amesema.
Aidha, ameeleza kuwa mashindano hayo yanatekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na Dira ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga mtaji wa watu wenye ujuzi na uwezo wa kushindana duniani.
Pia ameongeza kuwa "Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Afudh Amir, ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenda Shanghai kuanzia Septemba 22–27, 2026 kwa programu ya waangalizi, ikiwa ni hatua ya kujifunza namna mashindano ya WorldSkills International yanavyoendeshwa na kujiandaa kwa ushiriki wa baadae".






Comments
Post a Comment