Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Katika kuhakikisha huduma bora ya maji inaimarika Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Musoma (MUWASA) yatembelea maeneo yaliyopata upungufu wa huduma ya maji sambamba na kusikiliza kero zinazowakabili wateja wake.
Zoezi hilo ni mojawapo ya kudumisha mahusiano na mawasiliano kwa wateja wa MUWASA likiongozwa na timu kutoka Idara ya usambazaji maji na usafi wa mazingira wakiwemo kitengo cha mahusiano.
Wateja hao wameshukuru ujio wa wataalam hao huku wakipongeza kurejea kwa huduma ya maji, lakini wameiomba mamlaka hiyo kuongeza jitihada za kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana kwa uhakika.
Sanjari na hayo wameiomba MUWASA kujitahidi kutoa taarifa mapema ili pale kunapotokea changamoto inayosababisha maji kukatika au kupungua, wajiandae na kuchukua hatua za dharura wakati wakisubiri huduma kurejea.
Vilevile wameiomba Wizara husika kuboresha miundombinu ili iweze kwenda sambamba na mabadiliko ya uhitaji kwa kuwa wateja wanaongezeka na matumizi ya maji yanaongezeka huku wakitolea mfano wa wananchi wengi hivi sasa wameondokana na matumizi ya choo Cha shimo na kutumia choo chenye kutumia maji mengi hali inayopelekea mahitaji kuwa makubwa.
Kwa Upande wake Kaimu Meneja wa MUWASA, Mhandisi Nkoba Boniphace, amesema mamlaka katika kuleta ustawi wa huduma kwa wateja imepokea changamoto na maoni ya wananchi na inaendelea kuyafanyia kazi.
Aidha Mhandisi Nkoba ameongeza kuwa MUWASA inaendelea na maboresho ya huduma Manispaa ya Musoma na mitaa ya jirani ili kuweza kurejesha huduma kwenye maeneo yenye mapungufu.
Ameainisha maeneo ambayo huduma imeanza kurejea kuwa ni maeneo ya Buhare, Bweri na Nyabange ambapo maboresho hayo yamelenga kuimarisha upatikanaji wa maji na kupunguza adha kwa wateja waliokumbwa na upungufu wa huduma.
Hadi sasa wataalamu wa MUWASA wanaendelea kutekeleza majukumu yao kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi na huduma ya maji inaimarika kwa wateja wa Manispaa ya Musoma na Nyabange.










Comments
Post a Comment