Na MASHAKA MHANDO, Tanga
Serikali imetoa maagizo kwa wizara na taasisi za utafiti nchini kuhakikisha zinakamilisha taratibu zote za kimataifa za kupata ithibati, ili dawa zinazotokana na mimea zikishapita maabara na kuzalishwa viwandani ziache kuitwa 'dawa za asili' na badala yake zitambulike kama dawa za kisasa kutoka Tanzania.
Maagizo hayo yametolewa leo Augosti 24 na Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, jana wakati akifunga kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi, na Ubunifu yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga kuanzia Agosti 18 hadi 24, mwaka huu.
Akifafanua kuhusu dhana hiyo, Dkt. Mwigulu alitolea mfano dawa ya kutibu tezi dume iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), akieleza kuwa kuendelea kuziita 'dawa za asili' kunawafanya baadhi ya watu kuwa na ukakasi na mashaka nazo, licha ya kuwa zimepitia michakato yote ya kimaabara kama dawa nyingine za kigeni.
"Tuendelee kufanya taratibu zote za kiutafiti na kupata ithibati. Hata hizi dawa zinazotoka nje kama Panadol zimetengenezwa kwa miti, na mingine wanaitoa huku Afrika. Sasa kama dawa imetengenezwa kiwandani Tanzania kwa nini tuiite ya asili? Hii ya asili tubakize kwa yule anayechimba mzizi na kuchemsha, lakini ikishapita maabara inapaswa kuitwa dawa kutoka Tanzania," alisisitiza Dkt. Mwigulu.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisisitiza uendelezaji wa bunifu mbalimbali, akibainisha kuwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Ubunifu wa Samia (Samia Innovation Fund) kumelenga kuhakikisha tafiti hazibaki kwenye makabati bali zinaingia sokoni na kuleta tija kwa wabunifu na Taifa kwa ujumla.
Akiunga mkono hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Sanaa na Utamaduni, Dkt. Mwigulu aliagiza kuwa Serikali lazima iwe mdau wa kwanza kununua na kutumia bidhaa zilizotengenezwa na wabunifu wa Kitanzania ili kuwajengea uwezo, akipongeza vipuri vya pikipiki na bajaji pamoja na mipira ya michezo iliyozalishwa nchini na kuonyeshwa kwenye maadhimisho hayo.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema wizara inatekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kubadilisha mitaala ya elimu ili ifikapo mwaka 2030, asilimia 100 ya elimu iwe imejikita kwenye ujuzi.
Profesa Mkenda alibainisha kuwa shule za amali zitaendelea kujikita katika kutoa ujuzi na ubunifu badala ya nadharia pekee, ili wanafunzi wajifunze masomo ya sayansi yatakayowasaidia kubuni suluhisho na kujiajiri mara wanapohitimu masomo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Sanaa na Utamaduni, Mhe. Husna Sekiboko, alimpongeza Rais Samia kwa utoaji wa fedha na miongozo thabiti inayoimarisha sekta ya elimu, huku akitoa wito kwa Maofisa Manunuzi wa Serikali kuwa mfano wa kwanza kununua bidhaa za wabunifu wa ndani ili kuwajengea imani wananchi wengine.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, alieleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamekutanisha jumla ya taasisi 91 zilizobadilishana uzoefu na kuonyesha bunifu zinazotoa suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi hapa nchini.



Comments
Post a Comment