RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempongeza na kumshukuru Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa maono yake ya muda mrefu ya kutumia Mto Rufiji kuzalisha umeme wa uhakika kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya Tanzania, akisema utekelezaji wa wazo hilo umefikia hatua ya kihistoria baada ya kukamilika na kuzinduliwa kwa Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa MW 2,115.
Akizungumza leo Agosti 22, 2026 wakati wa kuzindua kituo hicho, Rais Samia amesema maono ya Mwalimu Nyerere yaliendelezwa na viongozi wa awamu zilizofuata, waliokuwa na dhamira ya kuhakikisha wazo hilo linaendelea kuwa sehemu ya safari ya maendeleo ya taifa.
Amesema pamoja na Mwalimu Nyerere, anawashukuru Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, na Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuendeleza na kuenzi maono hayo.
Rais Samia amesema safari ya mradi huo haikuwa rahisi, kwani ulikumbana na upinzani wa ndani na nje ya nchi pamoja na changamoto mbalimbali katika awamu tofauti za uongozi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mwaka 2019/2020 ilichukua hatua ya kuendeleza mradi huo kwa kuhakikisha fedha zinapatikana, changamoto zinatatuliwa na utekelezaji unaanza.
“Tunamshukuru sana Dkt. John Pombe Magufuli kwa ujasiri aliouonesha,” amesema Rais Samia.
Aidha, ameitaja Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendeleza utekelezaji wa mradi huo hadi kukamilika, huku akiwashukuru mawaziri na viongozi mbalimbali waliosimamia mradi huo katika hatua tofauti.
Rais Samia amewataka Watanzania kujifunza kutokana na historia ya mradi huo kwamba maamuzi yenye maslahi kwa taifa yanapaswa kusimamiwa kwa uthubutu na uvumilivu hata pale yanapokumbana na changamoto.
“Tunapofanya maamuzi yenye maslahi kwa taifa, hatupaswi kukata tamaa kwa sababu njia ya kufanikisha imekuwa ngumu. Bali tunapaswa kuwa na uthubutu na ujasiri wa kuyasimamia maono na maamuzi yetu ili kufikia malengo tuliyojiwekea na manufaa tunayoyatarajia,” amesema.
Amesema kukamilika kwa mradi huo ni heshima kwa viongozi wote waliowahi kusimamia wazo hilo, akisisitiza kuwa maono ya Mwalimu Nyerere sasa yameacha alama kubwa katika historia ya maendeleo ya Tanzania.






Comments
Post a Comment