SERIKALI imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha umeme unaozalishwa katika Kituo cha Julius Nyerere (JNHPP) unafika kwa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini, baada ya kukamilisha na kuendelea na miradi mikubwa ya njia za kusafirisha umeme.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema uwekezaji huo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha ongezeko la uzalishaji wa umeme linaenda sambamba na uwezo wa gridi ya taifa kupokea na kusafirisha umeme huo kwa ufanisi.
Ndejembi ameyasema hayo leo Agosti 22, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere, kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Serikali inatambua kuwa kuongeza uzalishaji pekee hakutoshi, kwa kuwa umeme huo unahitaji njia imara za kuusafirisha kutoka kwenye vituo vya uzalishaji hadi maeneo mbalimbali nchini.
“Mheshimiwa Rais, hata hivyo, tunatambua kwamba kuongeza uwezo wa uzalishaji pekee haitoshi. Lazima tuwe na mtandao wenye uwezo wa kupokea na kusafirisha umeme wote kwenda maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” amesema Ndejembi.
Ndejembi amesema kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma kumeongeza uwezo wa kufikisha umeme unaozalishwa JNHPP kuelekea Dodoma na maeneo mengine.
Amesema matokeo ya uwekezaji huo yameonekana ndani ya muda mfupi, ambapo kiwango cha juu cha matumizi ya umeme nchini kimeongezeka kutoka MW 2,130 hadi MW 2,280 ndani ya siku tatu baada ya njia hiyo kuwashwa.
“Ni wiki iliyopita tu, kiwango cha juu cha matumizi ya umeme katika nchi yetu kilikuwa ni megawati 2,130. Lakini mara baada ya kuwasha line ile ya Chalinze-Dodoma, ndio tumefikia sasa kiwango cha juu cha megawati 2,280... hii ni ndani ya siku tatu tu,” amesema.
Waziri Ndejembi amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa njia ya Chalinze–Mkuranga–Kinyerezi, hatua inayolenga kuimarisha usafirishaji na usambazaji wa umeme katika Kanda ya Pwani, hususan maeneo yenye shughuli kubwa za viwanda.
Aidha, amesema ujenzi wa njia ya TAZA ya Iringa–Mbeya–Tunduma/Sumbawanga, yenye urefu wa zaidi ya kilomita 617, umefikia takribani asilimia 98.
Amesema pia mradi huo utakapokamilika utaunganisha Rukwa na gridi ya taifa na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.
Sambamba na hayo amesema ujenzi wa njia ya Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika unaendelea, huku mkandarasi akiwa tayari katika eneo la mradi.
Amesema njia hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha na kusambaza umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara, hivyo kuimarisha huduma ya umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kusafirisha umeme ili kuhakikisha ongezeko la uzalishaji kutoka JNHPP halibaki kuwa umeme unaozalishwa pekee, bali linafika kwa uhakika kwa wananchi, viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.
Hatua hiyo inaweka msingi wa Tanzania kuwa na mtandao imara zaidi wa umeme, unaoweza kuendana na ongezeko la uzalishaji na mahitaji ya nishati katika safari ya maendeleo ya Taifa.



Comments
Post a Comment