Na MASHAKA MHANDO, Tanga
SERIKALI imezindua rasmi programu mpya ya kitaifa ijulikanayo kama InnoIP Tanzania, inayolenga kuwasaidia wabunifu zaidi ya 5,000 nchini kulinda haki zao za miliki bunifu kisheria na kuzigeuza kuwa biashara zinazoingiza fedha na kutengeneza ajira, ili kuepuka wizi wa mawazo unaowaathiri wabunifu wengi wazawa.
Uzinduzi huo wa kihistoria umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian Leo Augosti 22 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi, na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Usagara jijini Tanga, hafla iliyobebwa na kaulimbiu isemayo; "Kutoka Wazo hadi Fursa za Miliki Bunifu: Kulinda Ubunifu, Kujenga Thamani na Kuharakisha Ubiasharishaji".
Akihutubia mamia ya wadau wa sekta ya sayansi na ubunifu, Mkuu wa Mkoa alisema Tanzania lazima ihakikishe ubunifu wa ndani unalindwa na kuunganishwa na masoko makubwa, ili kuepuka hasara inayosababishwa na wabunifu kuweka wazi mawazo yao mapema mno kwa umma kabla ya kuyalinda kisheria.
Dkt. Batilda alibainisha kuwa hali ya wabunifu kuweka wazi mawazo yao bila makubaliano yanayoeleweka kuhusu umiliki, inamkosesha mbunifu fursa ya kupata ulinzi wa kazi yake, na inawafanya wawekezaji wasite kumwaga mitaji yao iwapo kampuni changa haithibitishi umiliki wake kisheria.
Sambamba na uzinduzi wa InnoIP, Mkuu wa Mkoa alitangaza pia kuanza kwa programu ya 'Fursa Women', inayolenga kuwainua wanawake wajasiriamali kwa kuwapa ujuzi wa kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali ili kukuza biashara zao, akisisitiza kuwa teknolojia hupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza wateja haraka.
Katika kuhakikisha mafanikio ya mipango hiyo, Mkuu wa Mkoa alitoa maagizo mazito kwa Vyuo Vikuu na taasisi za utafiti nchini kuhakikisha wanatengeneza bidhaa halisi zinazonufaisha jamii badala ya kuziacha tafiti zikioza kwenye makabati, huku akiwaasa wawekezaji na taasisi za fedha kushirikiana na wabunifu wa Kitanzania kwa kununua bidhaa zao na kuwapa mitaji.
Kwa upande wake, akizungumzia ushiriki wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika programu hiyo, Mkurugenzi wa Miliki akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, Loy Mhando alieleza kuwa programu hiyo haimaanishi kuwa kila ubunifu lazima upatiwe Hataza (Patent), bali inamsaidia mbunifu kutambua mbinu sahihi za ulinzi ikiwemo alama za biashara, hakimiliki, na siri za biashara.
Alifafanua kuwa InnoIP inasimamiwa na BRELA ikiratibiwa na COSTECH kupitia atamizi za Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) na Buni Innovation Hub, ambapo itawasaidia kampuni changa, watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu, biashara ndogo na za kati, na wajasiriamali kutambua, kulinda, na kubiasharisha haki zao za miliki bunifu.
Alieleza kuwa katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, programu hiyo inalenga kufanya uchambuzi wa mahitaji ya kina kwa wabunifu 120 wa mwanzo, ambao watasaidiwa kisheria na kifedha kulinda kazi zao, kisha kuunganishwa na wawekezaji, ambapo wabunifu hao watapatikana kwa kuzingatia vigezo vya umuhimu wa ubunifu husika kwa jamii na uwezo wa kuingiza faida.
Alisema kuwa programu hiyo itawasindikiza wabunifu kupitia hatua saba ikiwemo utambuzi na uhamasishaji, mafunzo na warsha za vitendo, uchambuzi wa mahitaji, maandalizi ya ramani ya ulinzi, kuwasilisha maombi ya usajili, ubiasharishaji kwa kuwatafutia wawekezaji, na hatimaye ufuatiliaji endelevu.
Mhando aliwataka wabunifu na kampuni changa nchini kutumia programu hiyo mapema na kutosubiri hadi mgogoro wa umiliki utokee, wazo linakiliwe na wajanja, au mwekezaji aanze kudai uthibitisho wa kisheria wa biashara zao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akitoa hotuba ya ukaribisho, alisema miliki bunifu si suala la kisheria pekee, bali ni rasilimali ya kiuchumi ambayo inaweza kuwa msingi mkuu wa kuvutia uwekezaji, kutoa leseni kwa viwanda vingine, kuhamisha teknolojia, na kujenga biashara kubwa zinazoweza kukua kimataifa.
"Changamoto yetu kuu kwa sasa nchini si ukosefu wa mawazo; ni kuhakikisha kuwa mawazo mazuri ya vijana, watafiti na wabunifu wetu yanalindwa kisheria, yanaendelezwa na hatimaye yanafikishwa sokoni," alisema Dkt. Nungu alipokuwa akisisitiza dhima kuu ya programu hiyo.
Mkurugenzi huyo wa COSTECH alisisitiza kuwa lengo kuu la programu hiyo si kuhesabu idadi ya watu waliohudhuria mafunzo na semina, bali matokeo ya InnoIP yatapimwa kwa kuona idadi ya ubunifu mwingi zaidi ukilindwa, teknolojia mpya zikiingia sokoni, biashara zikikua, uwekezaji mkubwa ukivutwa, na ajira nyingi mpya zikizalishwa nchini.
Akizungumzia Programu ya 'Fursa Women', Dkt. Nungu aliishukuru Kampuni ya simu ya Airtel Tanzania kwa ushirikiano wake na COSTECH katika kufadhili programu hiyo, akieleza kuwa ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa sekta ya umma na binafsi kufanya kazi pamoja katika kujenga jamii yenye ujuzi wa kidijitali.
Alifafanua kuwa kupitia Fursa Women, wanawake watajengewa uelewa kuhusu matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kidijitali katika kutangaza bidhaa, kuwafikia wateja wengi, kufanya na kupokea malipo mtandaoni, na kuhifadhi kumbukumbu za biashara zao.
Dkt. Nungu alihitimisha kwa kutoa wito kwa wawekezaji na sekta binafsi kutambua kuwa ubunifu wa Kitanzania ni fursa ya uwekezaji iliyolala, hivyo akawaalika kushirikiana na Serikali katika kujaribu, kununua, na kupanua matumizi ya teknolojia na suluhisho mbalimbali zinazozalishwa na Watanzania wazawa.
Maonesho ya wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanatarajiwa kufungwa Jumatatu na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.






Comments
Post a Comment