Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ndugu Fadhili Rajabu Maganya, ameendelea na ziara yake Wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu, kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti Maganya ameambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Ndugu Shamsa Mohamed, pamoja na viongozi na watendaji mbalimbali.
Akiwa Shule ya Msingi Meatu, Mwenyekiti Maganya amekagua ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa wenye thamani ya Shilingi milioni 125, unaolenga kuongeza nafasi za kujifunzia na kuweka mazingira bora kwa wanafunzi na walimu.
Aidha, ametembelea Shule ya Sekondari Meatu, ambako amekagua miundombinu ya shule hiyo na kupata taarifa kuhusu maendeleo pamoja na hali ya mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti Maganya pia ametembelea mradi wa ujenzi wa Nyumba ya Wazazi Wilaya ya Meatu pamoja na mradi wa vibanda vya Chama, ambapo amefuatilia hatua iliyofikiwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, kutambua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta manufaa kwa wananchi.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Jumuiya ya Wazazi Taifa ya kushirikiana na viongozi wa Chama na Serikali katika kusimamia maendeleo, hususan katika sekta ya elimu, ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.






Comments
Post a Comment