WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu, kilichopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, ni hatua muhimu katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kurahisisha huduma za forodha pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za mpakani.
Dkt. Nyansaho ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Kigoma, ambapo amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya kimkakati, ikiwemo Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu na ujenzi wa Barabara ya Kabingo–Kasulu Manyovu.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa na manufaa makubwa kwa Serikali na wananchi kwa kuwa kitaweka pamoja huduma mbalimbali zinazohusiana na shughuli za forodha, hivyo kupunguza usumbufu na kurahisisha utoaji wa huduma kwa watu wanaotumia mpaka huo.
Waziri Nyansaho, amesema uwepo wa kituo hicho unatarajiwa pia kuongeza ufanisi katika udhibiti wa shughuli zinazofanyika mpakani, sambamba na kuhakikisha Serikali inapata mapato yanayostahili kutokana na biashara na shughuli nyingine zinazofanyika katika eneo hilo.
“Ujenzi wa kituo hiki una umuhimu mkubwa kwa Taifa kwa sababu siyo tu utarahisisha utoaji wa huduma za forodha, bali pia utasaidia katika ukusanyaji wa mapato na kuimarisha usalama katika eneo hili la mpakani,” amesema Dkt. Nyansaho.
Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama, Waziri huyo amewataka wakazi wa Buhigwe kuendelea kuwa sehemu muhimu ya ulinzi wa nchi kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika kuhusu matukio au mienendo yoyote inayoweza kuhatarisha usalama.
Amesema usalama katika maeneo ya mipakani unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, viongozi na vyombo vya ulinzi na usalama, akisisitiza kuwa wananchi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama na tulivu.
Aidha, Dkt. Nyansaho ametoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu ya Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu mara kitakapoanza kutumika, akieleza kuwa miundombinu hiyo imejengwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Waziri Nyansaho amekagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kabingo–Kasulu–Manyovu, Lot 1 inayounganisha Kasulu na Manyovu kwa urefu wa kilomita 58.7.
Ameelezwa kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 100 na kwa sasa ipo katika kipindi cha matazamio, hatua inayodhihirisha kukamilika kwa sehemu hiyo muhimu ya miundombinu ya usafiri katika Mkoa wa Kigoma.
Barabara hiyo inatarajiwa kuendelea kuwa na umuhimu katika kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuunganisha maeneo ya ndani ya Mkoa wa Kigoma pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo.
Ziara ya Waziri wa Ulinzi na JKT Dkt. Nyansaho mkoani Kigoma ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati, kuhakikisha inakamilika kwa wakati na inatoa matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.



Comments
Post a Comment