Na MASHAKA MHANDO, Tanga
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umesema kuwa hatua ya mbunifu kusajili bidhaa au kazi aliyoibuni ni njia pekee na madhubuti ya kuitofautisha kazi hiyo na bidhaa bandia zinazoweza kuingizwa sokoni na wajanja kwa lengo la kujinufaisha isivyo halali.
Wito huo umetolewa na Afisa Usajili kutoka BRELA, Benedickson Willson, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga.
Willson amesema BRELA imeshiriki katika maonyesho hayo, yanayofanyika kuanzia Agosti 15 hadi 24 mwaka huu, kwa lengo la kuwafikia wabunifu na kuwaelimisha umuhimu wa kusajili kazi zao ili kupata haki ya kipekee ya kuzitumia na kuzilinda dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.
Akifafanua kuhusu ulinzi huo, Afisa huyo alisema kuwa usajili wa alama ya biashara na huduma humwezesha mmiliki kulinda chapa yake, huku akisisitiza kuwa ukiwa umesajili alama yako unakuwa na uwezo wa kisheria wa kuzuia bidhaa bandia kutumia chapa yako bila kibali, jambo linalolinda thamani ya kiuchumi ya ubunifu husika.
Ameongeza kuwa usajili huo unampa mbunifu fursa ya kutumia mali hiyo kibiashara, ikiwemo kuingia makubaliano na taasisi nyingine, au hata kuuza haki ya kutumia chapa yake kwa mtu mwingine kupitia makubaliano rasmi ya uhamishaji wa haki na kujipatia mamilioni ya fedha.
Willson alitolea mfano ubunifu unaohusisha teknolojia mpya, kama vile vifaa vya akili bandia (AI) au vinavyosaidia watu wenye ulemavu wa kuona, akibainisha kuwa teknolojia hizo zina uwezo mkubwa wa kuwa mali yenye thamani kubwa kibiashara ndani na nje ya nchi endapo zitasajiliwa ipasavyo.
Aliongeza kuwa watu wengi wanachukulia ubunifu kwa mtazamo wa kawaida, lakini ndiyo njia sahihi ya kuendeleza Taifa na kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, huku akiwataka vijana kutokubali kazi zao zitumike na watu wengine bila wao kupata manufaa yanayostahili.
Alihitimisha kwa kueleza kuwa ushiriki wa BRELA katika maonyesho hayo ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ubunifu unavyoweza kubadilishwa kuwa fursa ya kiuchumi, hivyo akawakaribisha wabunifu wote kufika kwenye banda lao ili wapate huduma na kuhakikisha ubunifu wao unatambuliwa na kulindwa.






Comments
Post a Comment