NA: MWANDISHI WETU
Wazazi na walezi waishio wilayani Pangani mkoani Tanga, wamehimizwa kuwapeleka watoto wao walio chini ya umri wa miaka kumi katika vituo vya kutolea huduma ili wakapate chanjo ya ugonjwa wa Polio.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Pangani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Agosti 25, 2026.
Amesema, chanjo hiyo ni muhimu kwani inawapa watoto hao kinga dhidi ya kupooza katika ukuaji wao na hivyo kuwaimarisha kiafya.
"Nitoe rai kwa wazazi na walezi, kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo ya Polio kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026. Hii itawasaidia watoto wao kuwa na afya na ukuaji bora," amesema Aweso.
Ameongeza kuwa, serikali inaandaa taifa la watu wenye afya bora, ndiyo maana inagharamia chanjo za magonjwa mbalimbali na kutoa bure kwa wananchi wake.
"Serikali inataka raia wake wawe na afya njema, ndiyo maana inasimamia kikamilifu utoaji wa chanjo za magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa Polio. Chanjo hii inawalinda watoto dhidi ya kupooza, ulemavu na hata kupoteza maisha," amesema.
Kimsingi, Halmashauri ya wilaya ya Pangani imejipanga kutoa chanjo katika vituo vyote vya afya, shule za msingi na awali, maeneo ya mikusanyiko pamoja na kaya kwa kaya.
Kampeni ya utoaji chanjo inaratibiwa na Wizara ya Afya ambapo kwa awamu hii itatolewa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Pwani na Tanga kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026.
Kampeni hiyo inachagizwa na kaulimbiu isemayo "Mpe Chanjo, Zuia Polio," ikihimiza watoto kupewa chanjo ili kujikinga na ugonjwa huo.

Comments
Post a Comment