Siasa za Ulimwengu Zinaathiri Nchi za Sadc

GEORGE MARATO TV
0


Hali ya sasa ya siasa za ulimwengu na vita zinazoendelea Mashariki ya kati, imesababisha madhara makubwa ulimwenguni ikiwemo kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na huo ni ujumbe tosha kwa nchi zetu kuchukua hatua Madhubuti za pamoja kujinasua.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC ambaye ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola, wakati akifungua mkutano wa 47 wa Baraza hilo unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini Machi 12 na 13, 2026.


Mhe. Lamola alisema hali hiyo inatishia mwenendo wa mnyororo wa biashara kwa  kupanda kwa gharama za mafuta duniani, suala ambalo litasababisha kupanda kwa gharama za mbolea na hatimaye bei za vyakula kuwa juu.  Hali hiyo ameitaja kama ni ya hatari kwa usalama wa chakula katika kanda ya SADC ikizingatiwa watu takribani milioni 58 wanakabiliwa na changamoto ya usalama wa chakula.

Alisema kutokana na vita hivyo, kuna uwezekano mkubwa nchi za Mashariki ya kati kuachana na mipango ya kuwekeza nje ya nchi ili kujikita na masuala ya usalama wa ndani. Hali hiyo ameilezea kuwa itakuwa na athari kubwa katika ukanda wa SADC, hususan kwenye sekta za miundombinu, fedha, teknolojia, madini na nishati zinazotekelezwa kwa ushirikiano na nchi hizo.

Ameongeza kuwa matukio hayo ya vita yanayoendelea, yatapunguza jitihada za viongozi wa nchi za Afrika kutafuta ufumbuzi wa madeni katika majukwaa ya kimataifa ambayo yanaelezwa kuwa, malipo yake kwa mwaka kwa nchi nyingi za Afrika, yanazidi bajeti ya elimu na afya.

Amewataka Mawaziri kutumia mkutano huo kupanga mikakati sahihi ya kukuza uchumi kwenye kanda ya SADC ambayo bado inakabiliwa na athari za janga la Ugonjwa wa COVID na vita vya Ukraine na Urusi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo akiambatana na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top