WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane 2026 ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika, huku yakitoa fursa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa maliasili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Akizungumza leo baada ya kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Dkt. Kijaji amesema wizara imeandaa huduma na maonesho mbalimbali yanayowapa wananchi, hususan wanafunzi, nafasi ya kujifunza kuhusu rasilimali za taifa na kushuhudia baadhi ya wanyamapori hai ili kuongeza uelewa kuhusu urithi wa asili wa Tanzania.
"Tupo hapa kwenye Maonesho ya Nanenane tukiwa tumewaletea wananchi huduma mbalimbali. Tunatoa elimu kuhusu uhifadhi na ustawi wa maliasili, lakini pia tumewaleta baadhi ya wanyamapori hai ili wananchi na wanafunzi wapate fursa ya kuwaona na kujifunza kuhusu utajiri mkubwa ambao Mwenyezi Mungu ameijalia Tanzania," amesema Dkt. Kijaji.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea wananchi hamasa ya kutembelea hifadhi za taifa, mapori ya akiba na vivutio vingine vya utalii vilivyopo nchini badala ya kuviona katika maonesho pekee.
Aidha, Waziri Kijaji amesema Maonesho ya Nanenane yanatoa fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya utalii, pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya sekta hiyo.
Amebainisha kuwa, licha ya utalii wa ndani kuendelea kukua, bado Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaotembelea vivutio vyao, sambamba na kuendelea kuvutia watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
"Utalii wa ndani unaendelea kukua, lakini bado haujafikia kiwango kinachoridhisha. Ndiyo maana tumekuja hapa kuwaelimisha wananchi na kuwahamasisha kutembelea vivutio vyetu vya utalii," amesema.
Dkt. Kijaji ameeleza kuwa kampeni hiyo inaendana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo imeweka lengo la kufikisha idadi ya watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
"Hii ni moja ya njia muhimu tunayoitumia kuhakikisha tunafikia lengo hilo kwa kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa kimataifa," amesisitiza.
Ziara ya Waziri Dkt. Kijaji katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii inayolenga kuwahamasisha Watanzania Kufanya utalii wa ndani ili kujionea rasilimali zilizopo nchini Tanzania pamoja na kuendelea kuitangaza Tanzania duniani kama moja ya maeneo bora ya utalii, huku akiwahamasisha Watanzania kutembelea na kuthamini vivutio vyao vya asili.




Comments
Post a Comment