Mwandishi Wetu Jovina Massano
Chama Cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA)na Chama Cha waandishi wa habari wa Ufalme wa Oman(OJA) kushirikiana katika kuibua fursa za kiuchumi kupitia habari.
Maamuzi hayo yametolewa mara baada ya ujumbe maalum kufika hapa nchini Agosti 19,2026 ukiongozwa na makamu Mwenyekiti wa OJA Salem Hamad Al-Jahwari.
Ujumbe huo umefanya mazungumzo na Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari (JOWUTA) pamoja na Serikali na kukubaliana kuandaa kongamano la kimataifa ambalo litahusisha wanahabari wa nchi hizo na sekta nyingine.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kitaalamu na kindugu, baina ya Oman na Tanzania, mazungumzo ambayo yamehudhuriwa na maafisa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari - Maelezo Jijini Dar es Salaam.
Ujumbe huo wa OJA, upo nchini kwa mwaliko wa JOWUTA, unaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa OJA.
Katika kikao hicho, Al-Jahwari ameeleza kuwa ziara hiyo inalenga kujenga nguzo thabiti za ushirikiano zitakazowezesha kubadilishana uzoefu, kutoa mafunzo ya kitalaamu, na kujengeana uwezo wa kiutendaji baina ya waandishi wa habari wa nchi hizo mbili.
Amebainisha kuwa ajenda kuu ya ziara hiyo ni kufanya majadiliano na uongozi wa JOWUTA pamoja na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya kongamano la pamoja la waandishi wa habari linalotarajiwa kufanyika hapa nchini baadaye mwaka huu.
Al-Jahwari amefafanua kuwa kongamano hilo linayalenga maeneo ya kimkakati ambayo ni biashara, uwekezaji, utalii na habari ili kuibua fursa za ushirikiano wa kiuchumi, litakuwa la pili kufanyika Barani Afrika baada ya lile lililofanyika nchini Misri.
Kongamano la aina hiyo limewahi kufanyika pia katika nchi za Uingereza, Marekani, China, na Uturuki.
Ikumbukwe kuwa Oman na Tanzania zina uhusiano wa kihistoria wa kindugu wa zaidi ya miaka 150.
"Tumeona ni busara kuja Tanzania kufungua milango ya ushirikiano wa moja kwa moja baina ya wanahabari wetu, kwani serikali zetu zina uhusiano wa kihistoria wa muda mrefu," alisema Al-Jahwari.
Nae Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-Maelezo Evod Kyando ameipongeza JOWUTA kwa hatua yake ya kupanua wigo wa ushirikiano na taasisi za kimataifa huku akisema juhudi hizo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kulitangaza Taifa kimataifa.
Ameongeza kuwa kongamano hilo linakuja wakati muafaka na litakuwa chachu ya kukuza uchumi kupitia sekta za kipaumbele za utalii, biashara na uwekezaji, jambo litakalochochea maendeleo ya nchi zote mbili.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, amesisitiza kuwa ushirikiano huo mpya kati ya JOWUTA na OJA utaleta tija kubwa kwa wanachama na waandishi wa habari kwa ujumla, hususan katika nyanja za mafunzo ya vitendo na kubadilishana uzoefu wa kiuhariri na kiuchunguzi.
“Sisi JOWUTA tunawashukuru OJA kwa kutambua uwepo wetu na kutushirikisha katika kuandaa kongamano hili la Kimataifa, tutahakikisha tunalitumia kuitangaza sekta ya habari na nchi yetu,” amesema, Selemani.







Comments
Post a Comment