PENYE SIASA ZA CHUKI NA MIVUTANO, BARAKA ZA MAENDELEO HUPOTEA," RAIS SAMIA ATOA ONYO KWA WANAOCHOCHEA VITENDO VYA UGAIDI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali, miundombinu na mienendo yoyote inayolenga kuyumbisha amani na usalama wa nchi pamoja na wananchi.
Amesema maslahi ya kisiasa, kiitikadi au kidini, havipaswi kutumiwa kama mwavuli wa vitendo vya kigaidi vyenye lengo la kutishia raia, kuharibu mali au kudhoofisha heshima ya nchi, akisisitiza kuwa maslahi ya watu wachache hayawezi kuwekwa juu ya usalama wa Watanzania.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akishuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar, kati ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha ACT Wazalendo, akisema hatua hiyo ni alama muhimu ya kuimarisha amani, umoja na utulivu wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
Amempongeza Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo kwa kutanguliza maslahi ya nchi katika kutafuta muafaka wa pamoja kwa mustakabali wa Zanzibar.
Halikadhalika, amewapongeza Marais wastaafu wa Zanzibar; Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa usimamizi na busara zao katika kufikia maridhiano hayo.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema maridhiano yaliyofikiwa ni kielelezo cha ukomavu wa kisiasa, uvumilivu na dhamira ya viongozi kutanguliza maslahi ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
"Maridhiano si udhaifu, bali ni ukomavu wa kisiasa unaojenga misingi ya umoja na kuheshimiana," amesema Rais Dkt. Samia, akiongeza kuwa "Zanzibar ikiwa na amani, Tanzania inakuwa salama."
Amesema wananchi hawahitaji mivutano ya kisiasa isiyoisha, bali mazingira ya Usalama na amani yatakayowezesha ustawi wa shughuli zao za kijamii, kiuchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi zote zenye nia ya kulinda amani na kuendeleza umoja wa Muungano wa Taifa letu.
Halikadhalika, amewataka viongozi na wananchi kuyalinda makubaliano hayo kwa vitendo, staha, uaminifu na kuendelea kuaminiana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema tamko hilo linafungua njia ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Ameongeza kuwa, hatua hiyo inaashiria kuanza kwa mazungumzo kuhusu ajenda zilizokubaliwa, kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za kisiasa Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema mchakato huo utaongeza imani ya wananchi, wawekezaji, wafanyabiashara na washirika wa maendeleo, akiwataka viongozi na wananchi kuuunga mkono kwa maslahi mapana ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Mhe. Othman, amesema mazungumzo hayo yanalenga kuleta ufumbuzi wa kudumu katika kuboresha mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa masuala ya kisiasa, kiutawala na kitaasisi.
"Linapotokea tatizo lolote, njia sahihi ni kuzungumza," amesema Othman. "Mazungumzo ndiyo yanayojenga, yanayopanga na yanayoweza kuzaa jambo la kutekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa."
Amesema ACT-Wazalendo imeingia katika mchakato huo kwa dhamira njema na itaendelea kutanguliza maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, mabalozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa.









Comments
Post a Comment