📍Mkandarasi wa umeme apewa mkwara mzito kukamilisha njia maalum ya Majani Mapana hadi Chongoleani ifikapo Agosti
Na MASHAKA MHANDO, Tanga
WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amempa miezi miwili (hadi mwezi Agosti mwaka huu) mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme chini ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha anakamilisha njia maalum (*line*) ya kufikisha nishati ya uhakika katika eneo la mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) Chongoleani jijini Tanga.
Onyo hilo limetolewa leo na Waziri Ndejembi wakati wa ziara yake maalum ya kukagua maendeleo ya mradi huo wa kimkakati, ambapo alibainisha kuwa ingawa kwa sasa umeme upo, Serikali inajenga miundombinu hiyo ya dharura kutoka kituo kikubwa cha kupoza umeme cha Majani Mapana ili kuzuia changamoto za nishati mradi utakapoanza kazi.
Waziri Ndejembi alisisitiza kuwa kasi ya ujenzi wa mradi huo hairuhusu kusuasua kwa sekta ya nishati, kwani mafuta ghafi yanatarajiwa kuanza kuwasili Tanga mapema mwezi Agosti, huku meli ya kwanza ikitarajiwa kupakia mafuta hayo rasmi ifikapo Januari 2027.
"Nimeridhishwa na hatua mbalimbali za ujenzi zilipofikia, hivyo nimemuagiza mkandarasi wa TANESCO kuhakikisha ile line maalum inakamilika ifikapo mwezi wa nane kulingana na mkataba wake. Akishindwa, tutamtoa na kumfungia kufanya kazi na TANESCO kwa sababu atakuwa amefeli, kwani katika miradi yote iliyopo hapa, yeye pekee ndiye bado yuko nyuma," alipiga mkwara Waziri Ndejembi.
*Ujenzi wa Bomba Wafikia Asilimia 90*
Akitoa ripoti ya maendeleo ya mradi huo mbele ya Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP, Guillaume Dulout, alitangaza mapinduzi makubwa ya kiufundi akibainisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya bomba hilo umekamilika kwa asilimia 90.
Dulout alieleza kuwa jumla ya kilomita 1,536 za bomba zimekwisha lala chini ya ardhi katika mikoa minane na wilaya 27 nchini Tanzania na Uganda.
"Hatua ya ujenzi imefikia hatua kubwa sana. Takriban kilomita 1,400 ambazo ni sawa na asilimia 91 ya urefu wote zimeshafunikwa na kurudishiwa udongo, ambapo bomba hili limelazwa katika kina cha angalau futi 6 chini ya ardhi katika maeneo yote ili kuimarisha usalama," alisema Dulout.
Aliongeza kuwa mradi huo unaohusisha jumla ya vituo sita (vinne nchini Tanzania na viwili nchini Uganda), kwa sasa umeingia rasmi katika hatua ya mwisho ya majaribio na makabidhiano ya mitambo kitaalamu (*Commissioning Phase*), ambapo kazi kubwa ya makabidhiano ya vifaa inafanyika.
*Uwekezaji wa Mabilioni na Hisa za Mataifa*
Kitalamu, mradi huu unatajwa kuwa mradi wa kwanza mkubwa duniani wa bomba refu la mafuta linalopashwa joto (Longest Electrically Heated Pipeline) lenye urefu wa kilomita 1,400.
Mradi huo una thamani ya uwekezaji wa Shilingi Bilioni 995 ambapo Serikali ya Tanzania imeweka Shilingi Bilioni 973 kupitia hisa za Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) linalomiliki asilimia 15 ya mradi. Ushirikiano mwingine unahusisha Serikali ya Uganda kupitia UNOC (15%), Kampuni ya TotalEnergies (65%), na CNOOC ya Uchina inayomiliki asilimia 8.
*Neema ya Ajira 18,000 na Uwanja wa Coastal Union*
Katika hatua inayofurahisha jamii, mradi huo umekuwa chachu ya ajira ambapo zaidi ya Watanzania 18,000 wamepata fursa za kazi, wakiwemo wakazi zaidi ya 5,000 kutoka katika jamii zinazozunguka mradi katika Kata ya Chongoleani jijini Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kusimamia mradi huo na kueleza kuwa mkoa umejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanachangamkia fursa zote za huduma.
Dkt. Batilda alitangaza neema ya kipekee kwa wapenzi wa michezo mkoani hapa, akibainisha kuwa kupitia wajibu wa mradi huo kwa jamii (*Corporate Social Responsibility - CSR*), wakazi wa Tanga watajengewa uwanja wa kisasa wa michezo utakaotumiwa na Timu ya soka ya klabu ya Coastal Union 'Wagosi wa Kaya'.




Comments
Post a Comment