Na MASHAKA MHANDO, Tanga
SERIKALI imeshauriwa kuanza kuingia mikataba ya kununua na kuwekeza kwenye teknolojia na bidhaa zinazobuniwa na vyuo vya elimu ya juu nchini, badala ya kutegemea zaidi kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu yanayofanyika mkoani Tanga.
Mhe. Sekiboko amesema hatua ya Serikali kutumia bunifu za ndani itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa kiteknolojia, kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, kuchochea ajira kwa vijana, na kukuza mapato ya Taifa kupitia bidhaa zenye nembo ya "Made in Tanzania".
Akithibitisha uwezo wa vyuo vya ndani kufanya mapinduzi, Mhe. Sekiboko alisema amevutiwa sana na kiwango cha tafiti zinazofanywa, akitolea mfano ubunifu uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Chuo hicho kimebuni na kuonyesha teknolojia ya uchunguzi wa afya ya mama mjamzito na mtoto tumboni (Ultrasound) inayolenga kutoa huduma kwa gharama nafuu zaidi.
Alisema ubunifu kama huo ni uthibitisho tosha kuwa vyuo vikuu nchini vina uwezo wa kuzalisha teknolojia thabiti za kutatua kero za wananchi, zinazoweza kutumika ndani na hata kuuzwa nje ya nchi.
Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kuongeza uwekezaji katika tafiti hizo na kuziunganisha taasisi za elimu ya juu na masoko, ili bidhaa zinazozalishwa ziwafikie wananchi moja kwa moja.
Ameongeza kuwa endapo Serikali, vyuo vikuu, na sekta binafsi zitaunganisha nguvu, Tanzania itatoka kwenye hatua ya kuwa "soko la wengine" na kuwa taifa linalotengeneza na kuuza teknolojia zake lenyewe.
Kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, Mhe. Sekiboko amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Tanga na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo ili kujionea, kujifunza, na kuchangamkia fursa za kiteknolojia zinazooneshwa na taasisi za elimu nchini.






Comments
Post a Comment