Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, leo Agosti 20, 2026, ametembelea na kujionea shughuli za Mashindano ya Ujuzi Kitaifa 2026 yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo la mashindano hayo, Prof. Nombo amesema Serikali inaendelea kutumia mbinu mbalimbali kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, ikiwemo kuwapa fursa ya kujifunza katika mazingira halisi ya kazi na viwandani, badala ya kutegemea mafunzo ya darasani pekee.
Amesema Mashindano ya Ujuzi Kitaifa yanafanyika kwa kuzingatia vigezo na viwango vya kimataifa, hivyo kuwapa washiriki fursa ya kuonyesha umahiri wao kwa kutumia viwango vinavyotambulika kimataifa.
Prof. Nombo amesema jambo lililomfurahisha zaidi katika maandalizi ya mashindano hayo ni ushirikiano uliopo kati ya taasisi za elimu na sekta ya viwanda, ambapo sehemu kubwa ya wataalamu na majaji wanaoshiriki katika mashindano hayo wanatoka katika sekta ya viwanda.
“Nikiongelea viwanda, si kiwanda ambacho kuna mashine pekee; tunaongelea namna tunavyowatoa wanafunzi darasani na kuwapeleka katika maeneo halisi ya kazi. Hii ni mbinu nyingine ya kumfanya mwanafunzi aweze kupata ujuzi unaotakiwa,” amesema Prof. Nombo.
Aidha, Prof. Nombo amesema mashindano hayo yanafanyika kwa hatua mbalimbali, ambapo washiriki wanashindanishwa katika fani tofauti kwa lengo la kubaini wenye uwezo na umahiri zaidi ambao watawakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
“Tunawaona vijana wetu wameweza kuonyesha ujuzi halisi wa yale ambayo wamefundishwa vyuoni. Tunategemea hawa walioko hapa wafanyiwe tathmini ili tupate vijana ambao wataweza kuiwakilisha nchi yetu katika Mashindano ya Ujuzi Afrika,” amesema.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kuhakikisha vijana wanapata fursa ya kuonyesha umahiri na ujuzi wao kwa kiwango cha juu, ili kuiwakilisha nchi katika majukwaa ya kimataifa na kuifanya dunia itambue uwezo wa vijana wenye ujuzi kutoka Tanzania.
Kwa upande mwingine, Prof. Nombo amelipongeza Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kuratibu Mashindano ya Ujuzi Kitaifa 2026, akieleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kuratibu mashindano hayo hadi kufikia ngazi za kimataifa.








Comments
Post a Comment