BUNIFU ZA KISHINDO TANGA: MUHAS YAGUNDUA DAWA YA TEZI DUME, CHUO CHA NELSON MANDELA CHAGEUZA KOROSHO KUWA KEMIKALI YA NGOZI
Na MASHAKA MHANDO, Tanga
Vyuo Vikuu nchini vimekuja na majibu ya vitendo dhidi ya changamoto za kiafya na kiuchumi zinazoikabili jamii, baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kugundua dawa ya kinga na tiba ya ugonjwa wa tezi dume, huku Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ikibuni kemikali ya kusindika ngozi inayotokana na maganda ya korosho.
Bunifu hizi za kihistoria zimebainishwa jijini Tanga wakati wa Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea jijini humo kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Usagara.
Akielezea ugunduzi huo wa kimatibabu, Daktari kutoka MUHAS, Dkt. Benson Peter, amesema chuo hicho kimefanya tafiti za kina tangu mwaka 2006 na kugundua mmea wenye kemikali zinazoweza kutibu tezi dume, mgonjwa akapona kabisa.
Matokeo ya utafiti huo yamezaa dawa iliyopewa jina la Brucan, ambayo tayari imetengenezwa katika mfumo wa vidonge na kuanza kutumika kwa wagonjwa na hata wasiokuwa wagonjwa kwa ajili ya kinga.
Dkt. Benson amebainisha kuwa dawa hiyo imeanza kutumika na kuleta matokeo chanya, ikiwemo kuzuia uvimbe, kukomesha tatizo la kwenda haja ndogo mara kwa mara, na kuwaponya kabisa wagonjwa.
Amewashauri wanaume kuanzia umri wa miaka 50 (ambao ndio waathirika wakubwa) kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua tatizo hilo mapema kabla halijabadilika na kuwa saratani.
Katika hatua nyingine, Mhadhiri na msomi kutoka Taasisi ya Nelson Mandela (NM-AIST), Dkt. Cecilia China, ameonyesha maajabu ya kiubunifu kwa kutumia maganda ya korosho kuzalisha kemikali mbadala kwa ajili ya usindikaji wa ngozi nchini.
Dkt. Cecilia ndiye mwanzilishi wa kampuni changa ya Afritek Organic Leather Company LTD, iliyopo chini ya NM-AIST, ambayo imelenga kuleta mapinduzi kwenye mnyororo wa thamani wa zao la korosho na sekta ya ngozi.
Akiwa mnufaika wa ufadhili wa Serikali, Dkt. Cecilia alishinda kiasi cha Shilingi milioni 20 mwaka 2019 kupitia Mashindano ya Ubunifu ya MAKISATU (chini ya COSTECH). Leo hii, ni mmiliki wa kiwanda jijini Arusha kinachotoa ajira kwa vijana na wanawake.
Dkt Mchina ana mpango wa kuanzisha kiwanda kikubwa zaidi mkoani Mtwara ili kukabiliana na changamoto ya usafiri kusafirisha malighafi kutoka Kusini kwenda kaskazini kilipo kiwanda chake kidogo
Alisema kujenga kiwanda Mtwara kitawasaidia wakulima kuingiza kipato mara mbili—kwa kuuza korosho yenyewe na pia kuuza maganda yake kama malighafi ya kiwanda hicho.
Ubunifu huo wa Dkt. Mchina unatajwa kuwa na uwezo wa kuokoa sekta ya ngozi nchini kwa kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo, usindikaji bora wa ngozi utaongeza thamani ya bidhaa hizo na kuingiza fedha za kigeni zinazohitajika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (kujenga uchumi wa Trilioni moja ya Dola za Marekani).
Akiishauri Serikali, Dkt. Cecilia aliitaka Wizara ya Elimu kuendeleza utaratibu wa kuibua kazi za wabunifu kupitia maonesho kama haya, na kuzitumia bunifu hizo kama suluhisho rasmi la matatizo ya wananchi na msingi wa kuanzisha viwanda vipya nchini.
Kisa cha MUHAS na Dkt. Cecilia ni ushahidi usiopingika kwamba kuwekeza kwenye hatua za awali za sayansi, teknolojia, na ubunifu kwa vijana ni kuwekeza katika ajira na uchumi wa Taifa.





Comments
Post a Comment