Na Mwandishi wetu Jovina Massano
Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara Juma Chikoka aja na mkakati wa kuinua elimu mpango ambao utashirikisha wazazi utakaowezesha safari salama ya elimu kwa wanafunzi lengo ni kuwajengea uelewa na kuongeza ufaulu wilayani hapa.
Akiongea katika kikao kazi cha tathmini ya elimu na viongozi wa Manispaa ya Musoma kilichowahusisha maafisa elimu,wenyeviti wa mitaa watendaji wa mitaa na Kata,maafisa maendeleo, vyombo vya ulinzi na usalama,waratibu elimu kata,madiwani,mstahiki Meya,Naibu Meya akiwemo na Mbunge wa Jimbo la Musoma.
Ameelezea kuwa mpango mkakati huo utakwenda kuchochea Maendeleo ya elimu kwa wanafunzi na kuongeza ubora wa elimu.
" Ushiriki wa wazazi/walezi na wadau wote ni muhimu katika safari ya elimu kwa wanafunzi kwa kuwa itasaidia kuongeza uelewa na ufaulu mzuri",amesema Chikoka.
Mpango huo unatokana na taarifa ya hali ya elimu ya awali na msingi iliyotolewa na kaimu afisa elimu wa Manispaa ya Musoma Pendo Tongora ikielezea changamoto zinazochangia kushuka kwa ufaulu.
Changamoto hizo ni uwepo wa utoro kwa wanafunzi, ushirikiano mdogo wa baadhi ya wazazi na walezi, chakula mashuleni ikiwemo upungufu wa walimu katika baadhi ya maeneo.
Kutokana na changamoto hizo Mkuu wa Wilaya amewaagiza makatibu elimu Kata kuhakikisha wanatoa tathmini ya elimu kila Ijumaa ikiwa ni sehemu ya hatua za ufuatiliaji kwa karibu mwenendo wa ufaulu wa wanafunzi katika Shule za msingi na sekondari.
Ili kufanikisha mpango huo amewasihi wazazi na walezi wote kushiriki kikamilifu na kuwa wafuatiliaji wa masomo ya wanafunzi pindi wanaporejea na pia kushiriki vikao mbalimbali vya Shule vitakavyokuwa vimeandaliwa mashuleni.
Aidha amesema kuanzia wiki inayofuata shule za msingi zitaanza mpango wa wanafunzi kusoma hadi sawa 11 jioni huku wakipatiwa chakula shuleni hatua ambayo inakenga kuongeza muda wa kujifunza na kuboresha ufaulu.
Hivyo ameagiza Shule zote kuitisha vikao vya wazazi huku akitoa wiki moja kwa wazazi kuchangia chakula Cha wanafunzi.
Kwa upande wa elimu ya sekondari wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi walio katika madarasa ya mitihani wataanza kukaa kambini kuanzia Septemba 1 ili kuwaandaa vizuri kuelekea mitihani ya kitaifa.
Kwa Upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma Alex Nyambiti amesema ili kuboresha matokeo ya wanafunzi kila mdau anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuwa elimu ni jukumu na pia ni jitihada za kila mmoja katika safari ya elimu yenye mafanikio.
Akimalizia Naibu Meya Haji Mtete amesema ushirikiano wa wadau wote kuanzia ngazi ya Serikali za mitaa,Kata, walimu na wazazi ni muhimu katika kuboresha sekta ya elimu.



Comments
Post a Comment