Na. MWANDISHI WETU, MWANZA
Serikali imedhamiria kuendelea kuimarisha afua za masuala ya UKIMWI nchini kwa kuboresha mazingira ya utekelezaji wa shughuli hizo, huku ikihimiza ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, alipotembelea na kujionea utekelezaji wa shughuli zinazotekelezwa na vikundi vya watu wanaoishi na Maambukuzi ya Virusi vya UKIMWI katika Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza.
Akiwa katika ziara hiyo, Dkt. Yonazi amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira na kutenga bajeti inayosaidia kuratibu na kutekeleza afua za masuala ya UKIMWI nchini, huku ikishirikiana na wadau mbalimbali.
“Ushirikiano ni muhimu sana kwani, tunaamini unauwezo wa kutuvusha katika mapambano dhidi ya VVU, ambapo tumeendelea kuunganisha nguvu pamoja katika mapambano hayo,” alisema Dkt. Yonazi.
Aliongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, yenye dhamana ya kuratibu shughuli zote za Serikali, ikiwemo masuala ya UKIMWI, itaendelea kuhakikisha vifaa na huduma zinatolewa kwa wakati na ubora kwa WAVIU, huku kanuni na taratibu za afya zikizingatiwa.
Dkt. Yonazi Ametumia jukwaa hilo kuiasa jamii kuendelea kupima afya ili kujitambua na kuchukua hatua za mapema endapo mtu atabainika kuwa na maambukizi ya VVU, ili aweze kuishi kwa tahadhari na kuwalinda wengine.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndugu Balandya Elikana, amesema kuwa mkoa umechukuwa hatua madhubuti kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na kamati za utekelezaji wa mikakati ya kuzuia maambukizi, huku wakihimiza upatikanaji wa huduma bora na elimu kwa jamii.
“Jamii inaendelea kuhamasishwa kuhusu upimaji wa afya kwa hiari na matumizi sahihi ya njia za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI pamoja na kuendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika na wadau wa afya ili kuboresha huduma za kinga na tiba,” alisema Elikana
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Kheri Kagya, akiwasilisha taarifa ya hali ya UKIMWI mkoani humo, amesema Mkoa wa Mwanza una kiwango cha maambukizi ya VVU cha asilimia 4.7, ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa cha asilimia 4.4, kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa THIS 2022/2023.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya DHIS2 Annual Report ya mwaka 2025/2026, Mkoa wa Mwanza unakadiriwa kuwa na idadi ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) 112,685.
“Mkoa, kwa kushirikiana na wadau, umeendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU kwa kuhamasisha matumizi sahihi ya kondomu. Katika kipindi cha mwaka 2025/2026, Mkoa ulisambaza jumla ya kondomu 2,265,772 katika jamii, hususani sehemu za kulala wageni, sehemu za kuuzia vileo (baa), kumbi za starehe na kwenye mikusanyiko mbalimbali,” alisema.

Comments
Post a Comment