Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

DC CHIKOKA AWAKUMBUSHA WAJUMBE WA KAMATI YA AFYA MSINGI (PHC)KUFANYA KAZI KWA UFANISI KUELEKEA ZOEZI LA UTOAJI CHANJO YA POLIO


 Na Mwandishi wetu Jovina Massano

MKUU wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara Juma Chikoka awakumbusha wajumbe wa kamati ya Afya ya msingi(PHC) Kufanya kazi kwa ufanisi kuelekea zoezi la chanjo ya Polio ya matone(nOPV2) linalitarajia kufanyika Agosti 27-30.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajumbe hao katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma ikiwahusisha washiriki kutoka halmashauri ya Musoma vijijini na halmashauri Manispaa ya Musoma.





Chikoka amesema kuwa katika halmashauri ya Musoma vijijini wanatarajia kuwafikia watoto walio chini ya miaka 10 wapatao 118,936 huku halmashauri ya Manispaa ya Musoma inatarajia kuwafikia watoto wapatao 66,176.

Amesema atahakikisha hamasa na elimu ya kutosha itatolewa kwa jamii ili kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu chanjo hii ambayo inakwenda kuondoa changamoto ya ulemavu kwa watoto.

"Tutaendelea kufanya ushirikishwaji na kushirikiana ili kuleta mapokeo na matokeo makubwa na kila mmoja atimize wajibu wake,"amesema Chikoka.

Ili kufikia mafanikio ya kampeni hiyo ushirikiano wa viongozi,wataalam wa afya,wahamasishaji na Jamii unahitajika kwa kiasi kikubwa.

Sarah Hussein Afisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na Anna Kajiru Afisa kutoka Wizara ya Afya Mpango wa Taifa wa Chanjo ni miongoni mwa wasimamizi wa utekelezaji wa zoezi hilo mpaka litakapokamilika.

Mratibu wa Chanjo hiyo wa halmashauri ya Manispaa ya Musoma Jamila Hassan amesema zoezi hili ni la awamu ya tatu na tayari ushirikishwaji umefanyika kuanzia ngazi ya mtaa hadi Wilaya lengo taarifa kuwafikia wananchi ili watoto wote lengwa wapatiwe chanjo hii.

Aidha wajumbe wa kamati hiyo wameiomba kamati ya ulinzi na usalama na viongozi kuweka mikakati maalum ya kuwafikia watoto wote wakiwemo wa mitaani.

Pia wameiomba Idara ya elimu na Idara ya afya kushirikiana katika kufikisha ujumbe wa kampeni hii ya chanjo kwenye Shule na Jamii kwa kuwapa taarifa na kuainisha walengwa wa zoezi hilo.

Ikumbukwe kuwa chanjo hii ni salama na imethibitishwa na kuidhinishwa na Shirika la Afya Duniani(WHO), Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba Tanzania (TMDA) hutolewa kupitia kampeni maalum inayohusisha mikakati ya nyumba kwa nyumba kwa kutembelea kaya zote,vituo vya kuyolea huduma ya Afya na maeneo ya mikusanyiko yaani nyumba za Ibada,Shuleni,Sokoni,na stendi.

Chanjo ya Polio ya matone (nOPV2) hutolewa kwa njia ya matone mawili mdomoni kwa kila mtoto alie kwenye kundi la umri lengwa bila kujali historia yake ya chanjo lengo ni kuimarisha kinga na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Polio aina ya pili katika jamii.

Akimalizia kwa kuielimisha jamii Kaimu Mganga mkuu wa Wilaya ya Musoma Ndulu Mahela amesema Polio ni ugonjwa hatari unaoweza kusababisha kupooza kwa ghafla kuliko teletepe,ulemavu wa kudumu hata kifo pia husababishwa na vidudu vya Polio aina ya 1,2 au ya 3 bao huenea kupitia kula chakulaaukunywa maji yenye vimelea vya Polio.

"Endapo kanuni za usafi hazizingatiwi katika jamii wadudu hak huingia mwilini kwa njia ya mdomo kwa kunywa au chakula ambacho kimechafuliwa na kinyesi kutoka kwa mwenye maambukizi ambapo vidudu kuongezeka ndani ya utumbo endapo kanuni za usafi wa mazingira hazijazingatiwa,"amesema Ndulu.

Hivyo basi ni muhimu kuimarisha na kudumisha usafi wa mazingira na usafi binafsi ili kujikinga na ugonjwa huo.

Ifahamike pia vidudu hivi vya Polio vinaweza kuathiri Neva za fahamu na kuleta athari za haraka katika mfumo wa upumuaji na kuweza kusababisha misuli ya viungo mbalimbali kulegea hali inayopelekea kupooza kwa ghafla au hata kifo ni muhimu kuchukua tahadhali mapema kabla ya kupata changamoto kubwa.

Wawakilishi kutoka UNISEF,BAKWATA na Baraza la Usuluhishi la wazee wameshiriki mafunzo hayo.





Comments