Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekagua Daraja la Mto Nyathorogo lililopo Kijiji cha Nyathorogo, Kata ya Nyathorogo, wilayani Rorya mkoani Mara, linalounganisha wilaya za Rorya na Tarime katika ziara yake ya kikazi mkoani humo leo Julai 2, 2026.
Akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Rorya, Mhandisi Elifadhili Moses, amesema ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 729.2, ambapo ulianza Agosti 1, 2025 na kukamilika Februari 28, 2026.
Mhandisi Moses ameeleza kuwa daraja hilo limejengwa kwa teknolojia ya mawe, hatua iliyosaidia kupunguza gharama za ujenzi kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na usanifu wa awali. Ameongeza kuwa Serikali tayari imetenga fedha katika mwaka wa 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa kingo za kulinda daraja hilo dhidi ya mmomonyoko wa maji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, amesema kukamilika kwa daraja hilo kumemaliza changamoto ya muda mrefu ya wananchi kuvuka Mto Nyathorogo katika mazingira hatarishi yaliyokuwa yakisababisha ajali na wakati mwingine vifo.
Amesema mradi huo umeimarisha mawasiliano kati ya wilaya za Rorya na Tarime, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.



Comments
Post a Comment