Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ametangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia utoaji wa kiasi cha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kupima vijiji vyote nchini ili kumaliza migogoro ya ardhi.
Mhe. Mmuya amebainisha hayo leo, Julai 1, 2026, katika viwanja vya Sokoni Mugumu wilaya ya Serengeti mkoani Mara, alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tano mkoani humo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi, zikiwemo zile za sekta ya ardhi.
Katika hatua ya haraka ya kusogeza huduma kwa wananchi, Mhe. Mmuya amemuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa wa Mara pamoja na timu yake, kuhakikisha wanaratibu na kuanzisha kliniki za ardhi katika kila kata na kila wilaya ya mkoa huo.
"Hakikisheni mnaratibu uwepo wa kliniki za ardhi katika kila kata, kila wilaya ili muwasikilize wananchi hawa na msione kila changamoto mpewazo ni ya mazoea. Hapana, amekuja kwako kwa sababu ana jambo la kusikilizwa na litatuliwe," alisema Naibu Waziri Mmuya.
Mhe. Mmuya alieleza kuwa wizara ya Ardhi iliwasilisha mpango na maombi ya fedha bungeni kufuatia maelekezo ya awali ya Waziri Mkuu, na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akaidhinisha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kupima jumla ya vijiji 12,333 vya Tanzania.
"Mpaka hivi ninavyoongea, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake kifupi tu ameweza kupima vijiji 4,873. Na ametupatia maelekezo kuwa ndani ya kipindi chake, vijiji vyote vilivyobakia tuvipime." Aliongeza Naibu Waziri Kaspar Mmuya
Katika hatua nyingine Mhe. Mmuya amesema Wizara ya Ardhi itashirikiana bega kwa bega na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kikamilifu katika vijiji vyote vilivyosalia nchini.
Aidha, Mhe. Mmuya alieleza kuwa Wilaya ya Serengeti ina kata 30 na vijiji 78. ambapo ameuhakikishia uongozi wa wilaya hiyo kuwa vijiji vyote 78 vimeshaingizwa kwenye mpango wa upimaji ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan.
"Kupima vijiji hivi ndiyo dawa kubwa ya kutatua changamoto ya mipaka kati ya kijiji na kijiji. Lakini ni dawa kubwa ya kutatua changamoto ya kugombania matumizi ya ardhi ya mtu mmoja mmoja, taasisi na taasisi, au serikali na wananchi," alisema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.







Comments
Post a Comment