Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Mary Surati, ameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, maji na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Serengeti ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na sekta ya utalii.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Serengeti uliofanyika leo Julai 1, 2026 mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Surati amesema wananchi wa eneo hilo wameendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda na kuhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ameeleza kuwa hifadhi hiyo ni miongoni mwa hazina kubwa za taifa, ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya fedha za kigeni na mapato ya serikali, hivyo kuiweka Serengeti katika nafasi ya kipekee kimataifa katika sekta ya utalii.
Aidha, ameshukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa maji unaoendelea, huku akiomba ukamilishwe kwa haraka ili kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ambapo ameomba wananchi wa Serengeti kupatiwa maji kutoka ziwa Victoria.
Kuhusu uwanja wa ndege wa kimataifa wa Serengeti, Mhe. Surati amesisitiza kuwa mradi huo ni muhimu kwa kukuza utalii na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, ameitaka Serikali kushughulikia malipo ya fedha za “open area”, akibainisha kuwa bado kuna malipo ambayo hayajakamilika licha ya maboresho ya kisheria yaliyofanyika, huku akisisitiza fedha hizo ni muhimu kwa shughuli za ulinzi wa hifadhi na malipo ya askari wa vijiji (village game scouts).
Pia ameiomba Serikali kuhakikisha fidia kwa wananchi wanaoathiriwa na wanyamapori inalipwa kwa wakati ili kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na taasisi za uhifadhi.
Sambamba na hayo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo na kuimarisha sekta ya uhifadhi nchini.
Amesema wananchi wa Serengeti wataendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda amani, hifadhi na maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa Serengeti itaendelea kuwa urithi muhimu wa Tanzania na dunia kwa ujumla.

Comments
Post a Comment