Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mheshimiwa Mary Daniel Surati, amewahimiza wazazi na walezi katika Wilaya ya Serengeti kutumia fursa ya Kliniki Maalumu ya Uchunguzi, Vipimo na Matibabu Bure kwa watoto wenye umri wa miaka 15 na chini.
Kliniki hiyo maalumu imeandaliwa kwa lengo la kuwawezesha watoto kupata uchunguzi na huduma za afya mapema, hususan kwa magonjwa ya Sickle Cell, figo na ini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mheshimiwa Surati, watoto watakaohudhuria kliniki hiyo watapatiwa uchunguzi, vipimo, dawa na matibabu bila malipo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha watoto wanapata huduma muhimu za afya kwa wakati.
Mheshimiwa Surati amewataka wazazi na walezi kutokosa fursa hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuwapeleka watoto wao kwa ajili ya uchunguzi wa afya hata pale ambapo hawajaonesha dalili kubwa za ugonjwa.
“Ninawasihi wazazi na walezi wenye watoto wanaokidhi kigezo hiki kutumia fursa hii muhimu ya kupata uchunguzi, vipimo na matibabu bila gharama,” amesema.
Ameeleza kuwa afya bora ya watoto ni msingi wa kujenga familia na jamii yenye nguvu, hivyo wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wao wanapata huduma za afya kwa wakati.
Kigezo cha kupata huduma: Mtoto anatakiwa kuwa na umri usi zaidi ya miaka 15.
Kwa mawasiliano na maelezo zaidi kuhusu kliniki hiyo, wazazi na walezi wanaweza kupiga simu kupitia 0766 730 305 au 0791 706 397.
Mheshimiwa Mary Daniel Surati amewakaribisha wananchi wa Serengeti kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo ya huduma za afya bure kwa watoto, akisema: “Tujenge Serengeti yenye afya bora kwa watoto wetu.”

Comments
Post a Comment