*"Nilipopata kazi yangu ya kwanza niliogopa kusema 'sijui'. Lakini CRJE ilitupatia mazingira mazuri. Wahandisi wakubwa walitufundisha kazini."*
Hayo ni maneno ya Mhandisi Titus Lukuwi wa kampuni ya CRJE, kijana ambaye alianza kama mfanyakazi wa kawaida mwaka 2022 na leo ni miongoni mwa wafanyakazi muhimu wa kiufundi katika miradi mikubwa ya ujenzi nchini.
Hadithi ya Lukuwi ilikuwa moja ya vivutio vikubwa katika "Mjadala wa China-Tanzania kuhusu Maendeleo na Ubadilishanaji wa Vijana" uliofanyika Dar es Salaam leo.
"Nilianza kazi nikiwa sijui chochote. Kupitia mafunzo ya CRJE mwaka 2023 na 2025, hatua kwa hatua nilijifunza ujuzi wa uhandisi, mawasiliano, utekelezaji wa miradi na viwango vya ubora," amesema Lukuwi.
"Leo niko katika timu inayotengeneza miundombinu ya ubora kwa Tanzania. Matumaini yetu ni kwamba katika miaka michache ijayo wahandisi wa Kitanzania watakuwa na uwezo wa kuongoza miradi kwa ajili ya kampuni na nchi yetu."
VIJANA WATAJWA KUWA MSINGI WA USHIRIKIANO
Akizungumza katika mjadala huo, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. CHEN Mingjian, amesema vijana kama Lukuwi ndio msingi wa mustakabali wa uhusiano kati ya China na Tanzania.
Mjadala huo umehudhuriwa na wawakilishi zaidi ya 100 kutoka serikali za China na Tanzania, vyuo vikuu, makampuni ya ujenzi, vyombo vya habari na wanafunzi. Unafanyika katika mwaka maalumu ambapo 2026 inatimiza miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika. Pia umetangazwa kuwa "Mwaka wa Ubadilishanaji wa Watu kwa Watu kati ya China na Afrika".
Akifungua mjadala huo, Balozi Chen amesema katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, China na Tanzania zimeandika historia nzuri ya udugu na ushirikiano. "Kuanzia ujenzi wa Reli ya TAZARA hadi Daraja la Nyerere, ushirikiano wetu umeweka watu katikati ya kila kitu," amesema Balozi Chen.
Ameongeza kuwa vijana ni nguvu muhimu katika kujenga "Jumuiya imara kati ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja". Ameeleza matumaini yake matatu kwa vijana: kuwa "wafuatiliaji wa ndoto", "daraja la kujifunzana" na "nguvu hai" ya maendeleo katika mafunzo ya ufundi stadi, ujenzi, uchumi wa kidijitali na uchumi wa kijani.
"Urafiki kati ya mataifa yetu unajengwa kwa mawasiliano ya watu kwa watu, na mawasiliano hayo yanategemea vijana," amesema Balozi Chen. Pia ametangaza kuwa Ubalozi utashirikiana na wadau kuongeza fursa za masomo ya udhamini na programu za ubadilishanaji wa vijana mwaka ujao.
*SERIKALI YATAKA UJUZI UWE KITOVU*
Kwa niaba ya Serikali, Dkt. Fredrick Salukele, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema ni wakati wa ushirikiano kubadilika kutoka miundombinu na biashara pekee, na kuelekea kuwaweka vijana, maarifa, ujuzi na uvumbuzi kitovu.
"Tanzania inatekeleza mageuzi ya elimu yanayolenga ujuzi na stadi za kidijitali. Ulimwengu wa kazi unabadilika kwa kasi kutokana na Akili Bandia. Tunapaswa kuwaandaa vijana kwa ajira za leo na kesho," amesema Dkt. Salukele.
Ametaka makampuni ya Kichina kujumuisha uhamishaji wa ujuzi katika uwekezaji wao kupitia mafunzo ya ufundi, utafiti, uvumbuzi na vyeti vya kitaaluma. "Lengo ni kubadilisha 'ubadilishanaji wa watu' kuwa 'ubadilishanaji wa ujuzi'," amesisitiza.
*VYUI NA MAKAMPUNI YATOA MIFANO*
Prof. Baraka J. Maiseli, Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano UDSM, ametoa mfano wa Chuo cha Huawei ICT ambacho kimewasaidia wanafunzi kupata ujuzi wa 5G, Akili Bandia na usalama wa mtandao. Alisema mwaka 2025 pekee wanafunzi 100 wa Kichina walikuja UDSM kusoma Kiswahili.
"Tunahitaji Mtindo wa Triple-Helix: Sekta ya Viwanda, Vyuo na Serikali kushirikiana kutengeneza ajira," amesema Prof. Maiseli. "Vijana wa Kichina na Watanzania wanapaswa kukaa pamoja na kutatua matatizo kwa vitendo. Jengeni ufumbuzi. Ongozeni miaka 60 ijayo."
Bw. JIANG YUNTAO, Mwenyekiti wa CRJE (East Africa), amesema katika miaka 50 iliyopita CRJE imeipa kipaumbele kukuza vipaji vya Watanzania. "Kuanzia TAZARA hadi Daraja la Nyerere, dhamira yetu ni kujenga watu pia, sio miundombinu tu," amesema.
Ametangaza mpango mpya wa "Mabwana wa Kichina, Urithi wa Kitanzania" wa mafunzo ya bwana-fundi. "Mhandisi wa Kichina anapomfundisha kijana wa Kitanzania, ndipo tunajenga urafiki wa kudumu," amesema. Ameahidi kuwa ndani ya miaka 10, wahandisi na viongozi wa Kitanzania wataongoza miradi mikubwa.
*SAUTI YA VIJANA*
Wanafunzi wa UDSM nao wamesema mjadala umewapa mwelekeo. Brian Samuel, mwanafunzi wa mwaka wa 3 CoICT, amesema: "Hatutaki vyeti tu. Tunataka kujenga miradi halisi, kujifunza kutoka kwa wahandisi kazini, na kupata vyeti vinavyohitajika na makampuni. Tuko tayari kuwa sehemu ya miaka 60 ijayo ya ushirikiano."
Mjadala huu umeandaliwa kwa pamoja na Xufang International Media ya CICG, CRJE, na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Comments
Post a Comment