Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa kuwekeza trilioni za fedha katika sekta za kimkakati zikiwemo umeme, maji, afya, elimu, kilimo, reli, barabara, bandari na usafiri wa anga.
Msigwa ameema mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa Tanzania inaendelea kujenga uchumi imara unaojitegemea, huku utegemezi wa misaada ya nje ukizidi kupungua kutokana na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Ameeleza kuwa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 yenye thamani ya Shilingi trilioni 62.33 ni bajeti ya kihistoria itakayokuwa msingi wa kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku asilimia 74.2 ya fedha zake zikitokana na mapato ya ndani.
"Kipindi cha miaka michache iliyopita tulikuwa tunategemea misaada kwa kiwango kikubwa, lakini leo Tanzania imefikia hatua ya kujitegemea kwa zaidi ya asilimia 74 ya bajeti yake. Haya ni mafanikio makubwa ya uongozi wa Awamu ya Sita," amesema Msigwa.
Amebainisha kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki ndani ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 3.4.
Msigwa amesema Serikali imewekeza nguvu kubwa katika sekta ya nishati ambapo uzalishaji wa umeme umeongezeka kwa kasi baada ya kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), pamoja na miradi mingine ya umeme wa maji, gesi na jua, hatua iliyomaliza tatizo la mgao wa umeme na kuongeza uwezo wa kuhudumia viwanda na wawekezaji.
Katika sekta ya kilimo, amesema Serikali imeongeza bajeti kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi Shilingi trilioni 1.19 mwaka 2025/26, huku zaidi ya wakulima milioni 2.8 wakinufaika na ruzuku ya mbolea iliyoongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Aidha, amesema Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi trilioni 3.4 katika miradi ya maji, hatua iliyoongeza upatikanaji wa maji safi vijijini hadi asilimia 85.2 na mijini kufikia asilimia 92.5, huku miradi mikubwa ya maji ikiendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa miundombinu, Msigwa amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), barabara, madaraja, viwanja vya ndege na maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, hatua zilizoongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria pamoja na kukuza biashara ya kikanda na kimataifa.
Amesema Bandari ya Dar es Salaam sasa inahudumia shehena nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali, huku muda wa kuhudumia meli ukipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na maboresho yaliyofanyika.
Katika sekta ya anga, Msigwa amesema Serikali imenunua ndege mpya 15 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16 zinazotoa huduma ndani na nje ya nchi, huku idadi ya vituo vya safari ikiongezeka kutoka 23 hadi 33.
Akizungumzia mahusiano ya kimataifa, Msigwa amesema ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imefungua fursa mpya za uwekezaji katika nishati, kilimo, utalii, elimu, usafiri wa anga na biashara, huku safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Moscow zikitarajiwa kuanza Julai 2, 2026.
Amesema Serikali pia imeimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Singapore pamoja na Namibia na inajiandaa kumpokea Rais wa Msumbiji Daniel Francisco Chapo ambaye atafanya ziara ya kikazi nchini Julai 2 hadi 3, 2026.
Msigwa amewahimiza Watanzania kuendelea kulipa kodi kwa hiari, akieleza kuwa mafanikio yote ya maendeleo yanatokana na mapato ya ndani pamoja na matumizi sahihi ya mikopo ya maendeleo.
Akizungumzia deni la taifa, amesema Serikali inakopa kwa ajili ya kuwekeza katika miradi yenye tija na si kwa matumizi ya kawaida, huku tathmini zikionesha kuwa deni la Tanzania bado liko ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa.
Ametaka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu hali ya uchumi na deni la taifa, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayoboresha maisha ya Watanzania na kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi imara na shindani ifikapo mwaka 2050.





Comments
Post a Comment