Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewashukuru wanachama wa CCM kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hatimaye kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi wa kishindo na kuendelea kuongoza dola Tanzania Bara na Zanzibar.
Dkt. Samia ameyasema hayo mara baada ya kukaribishwa na kuzungumza na wananchi pamoja na wanachama wa CCM katika Maskani Kaka Kisonge, Zanzibar.
Amesema jitihada zinazofanywa na wanachama katika kujenga umoja na mshikamano ndani ya maskani ni miongoni mwa mambo yanayomtia moyo, kwani zinaonesha kuwa wanachama wa CCM wako pamoja na wana dhamira ya kuendelea kukiimarisha chama kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Aidha, Dkt. Samia amesema Mapinduzi ni urithi walioachiwa na viongozi na wazee waliotangulia, hivyo kuna wajibu kwa kizazi cha sasa kuulinda, kuutunza na kuuendeleza ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwa na tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na huduma bora.
Amesisitiza kuwa wananchi wana wajibu wa kuyatunza, kuyaenzi na kuyasimamia maendeleo yanayopatikana, ili yaendelee kuwa na manufaa kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.




















Comments
Post a Comment