Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime na Diwani wa Kata ya Nyamisangura, Tobias Elias Ghati, amesema ziara ya madiwani wa halmashauri hiyo jijini Dodoma imekuwa ya mafanikio makubwa, ikiwapa nafasi ya kujifunza kwa kina utendaji wa Bunge na taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na kujionea miradi ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, Tobias amesema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kuimarisha uelewa wa viongozi wa serikali za mitaa kuhusu mfumo wa utawala na uwakilishi wa wananchi katika ngazi ya taifa.
Amesema awali madiwani walikuwa na matarajio ya kushiriki shughuli za kuapishwa kwa Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, lakini kutokana na changamoto za kiuratibu hawakuweza kufanikisha. Hata hivyo, baadaye walipata mwaliko kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, uliowawezesha kufanya ziara rasmi ya Bunge.
Tobias amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kipekee kushuhudia namna Bunge linavyofanya kazi, ikiwemo mijadala ya wabunge na namna sera na maamuzi ya maendeleo yanavyopitishwa.
Ameeleza kuwa uzoefu huo utawasaidia kuboresha utendaji wao katika kusimamia miradi na kuibua maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
"Tumejifunza kwa kina namna Bunge linavyofanya kazi na jinsi maamuzi yanavyofikiwa. Hii itatusaidia zaidi kuboresha utendaji wetu kwa wananchi," amesema.
Aidha, amebainisha kuwa walipata fursa ya kukutana na baadhi ya mawaziri na manaibu mawaziri ambapo waliwasilisha changamoto mbalimbali za halmashauri, hususan katika sekta za miundombinu, afya na elimu.
Amesema Serikali imeonesha mwitikio chanya na kutoa matumaini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo uboreshaji wa barabara kupitia TARURA pamoja na kuboresha huduma za kijamii.
"Tumepata mrejesho mzuri kutoka kwa viongozi wa Serikali. Changamoto zetu zimepokelewa na kuna matumaini ya hatua kuchukuliwa kwa wakati," ameeleza.
Ziara hiyo pia ilihusisha kutembelea Mji wa Serikali Mtumba, Relief ya Kisasa ya SGR pamoja na taasisi mbalimbali jijini Dodoma, ambapo madiwani walijifunza namna Serikali inavyopanga na kusimamia miundombinu na huduma kwa wananchi.
Baadaye, madiwani hao walihitimisha ziara yao kwa chakula cha pamoja kilichoandaliwa nyumbani kwa Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, ambapo walijumuika pia na Mbunge wa Viti Maalum Ghati Chomete pamoja na Mbunge Agnes Marwa.
Tobias amesema mkutano huo wa kijamii umeongeza mshikamano kati ya viongozi wa Mkoa wa Mara, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kuhusu kutokukutana na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, amesema hakuna mgogoro wowote, bali changamoto ilikuwa ni tofauti za ratiba.
"Hatuna mgogoro wowote. Tunaheshimiana na tunaendelea kushirikiana na viongozi wote. Tunaamini fursa nyingine zikipatikana tutakutana na kushirikiana kama kawaida," amessema.
Sambamba na hayo amewataka wananchi wa Tarime kuendelea kudumisha umoja na kushirikiana na viongozi wote bila kujali tofauti za kisiasa, akisema maendeleo yanahitaji mshikamano wa pamoja.






Comments
Post a Comment