WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa onyo kali kwa watu wanaovamia maeneo ya hifadhi nchini, akisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na uharibifu wa maliasili.
Waziri Kijaji ameyasema hayo leo Juni 25, 2026 jijini Dodoma Katika Mkutano wa Mwaka wa Wahifadhi Wanyamapori, unaofanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Uhifadhi Endelevu kwa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Taifa katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kijaji amesema sekta ya uhifadhi inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa zinazohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema moja ya changamoto kubwa ni ongezeko la migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu, hali inayosababisha uharibifu wa mashamba, makazi na mifugo, hususan katika maeneo ya vijijini.
Ameeleza kuwa hali hiyo inachangiwa zaidi na uvamizi wa maeneo ya hifadhi pamoja na matumizi ya ardhi yasiyozingatia mipango rasmi.
Waziri Kijaji ametaja ujangili na biashara haramu ya nyara za wanyamapori pamoja na mazao ya misitu kuwa ni tishio linaloendelea kuathiri uhai wa spishi mbalimbali na kudhoofisha sekta ya utalii nchini. Amesema uvami wa misitu ya vijiji na shoroba za wanyamapori waibua hofu
Aidha, ameeleza kusikitishwa na kasi ya uharibifu wa misitu ya vijiji na maeneo ya hifadhi, akisema baadhi ya maeneo yamegeuzwa kuwa mashamba kinyume cha sheria.
Ameonya pia kuwa uvamizi wa shoroba za wanyamapori umevuruga mfumo wa uhamaji wa wanyama na kuongeza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
Waziri Kijaji amesisitiza kuwa serikali haitavumilia uvamizi wowote wa maeneo ya hifadhi, akibainisha kuwa sheria zitatekelezwa bila upendeleo.
“Maeneo yote yaliyohifadhiwa lazima yabaki salama. Pale itakapobainika uvamizi, hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja bila kusita,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa uhifadhi endelevu ni msingi muhimu wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo kila mdau ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kulinda maliasili za taifa.
Mkutano wa Mwaka wa Wahifadhi Wanyamapori umefanyika Kwa mara ya pili ambapo Kwa mwaka huu 2026 unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Uhifadhi Endelevu kwa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Taifa katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”



Comments
Post a Comment