KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA YATEMBELEA HOSPITALI KUU YA JWTZ MSALATO
Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), tarehe 23 Juni 2026, ilifanya ziara katika Hospitali Kuu ya Kanda ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Msalato, jijini Dodoma, kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Katika ziara hiyo, Kamati ya NUU ilipokelewa na uongozi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ukiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho. Ziara hiyo ni sehemu ya jukumu la Kamati la kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo chini ya sekta ya ulinzi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya inayolenga kuboresha huduma za matibabu kwa wanajeshi, familia zao na wananchi kwa ujumla.
Kamati hiyo, ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Pascal Chinyele, ilitembelea maeneo mbalimbali ya hospitali na kujionea hatua za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mheshimiwa Pascal Chinyele alisema kuwa Kamati imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo na kuahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya NUU, Mheshimiwa Chinyele alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati, ambao unatarajiwa kuimarisha huduma za afya kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.










Comments
Post a Comment