Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesema litaendelea kutoa elimu ya kilimo bora na cha kisasa, ufugaji na uvuvi kwa wananchi hata baada ya kufungwa kwa Maonesho ya Wakulima (Nanenane), huku likiandaa mfumo maalumu wa kuwafuatilia na kuwawezesha vijana wanaohitimu mafunzo yake kujikita katika shughuli za uzalishaji na kujitegemea.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, alipotembelea banda la JKT katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Agosti 4, 2026.
Meja Jenerali Mabele alisema maonesho ya Nanenane ni fursa muhimu kwa JKT kuonyesha teknolojia na mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi, huku akisisitiza kuwa huduma hizo zitaendelea kutolewa hata baada ya maonesho hayo kumalizika.
"Kwetu sisi maonesho haya ya Nanenane ni endelevu. Hata baada ya maonesho haya kufungwa, tutaendelea kuwepo hapa na katika kanda zote ambazo JKT linashiriki ili wananchi waendelee kupata elimu ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa," amesema.
Aidha, alisema JKT linaweka utaratibu mpya wa kuwafuatilia vijana wanaomaliza mafunzo ili kufahamu maendeleo yao na kuwasaidia kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
Ameeleza kuwa hapo awali hakukuwa na mfumo rasmi wa kuwafuatilia wahitimu wa JKT, lakini sasa jeshi hilo linaandaa programu itakayowaunganisha na fursa za mafunzo, ushauri na mikopo kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji.
Meja Jenerali Mabele amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mafunzo yanayotolewa na JKT yanazaa matokeo ya muda mrefu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi pamoja na uchumi wa taifa.







Comments
Post a Comment