Waziri wa Fedha, Mhe. Khamis Mussa Omar, akiwa mgeni rasmi, amefungua Semina ya Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) kuhusu Bajeti yenye Mlengo wa Kijinsia iliyofanyika leo, tarehe 19 Juni 2026, katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma.
Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, Mhe. Omar amesema bajeti yenye mlengo wa kijinsia ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa wanawake, watoto na makundi maalum wanapata fursa sawa na kunufaika kikamilifu na utekelezaji wa mipango na matumizi ya rasilimali za umma.
Amesema kuwa utekelezaji wa bajeti hizo unachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza pengo la kijinsia, kupunguza umaskini na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa kuzingatia usawa na ujumuishi.
“Bajeti yenye mlengo wa kijinsia inatuwezesha kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo kwa kuzingatia mahitaji halisi ya makundi mbalimbali ya kijamii, huku ikihakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa usawa,” amesema Mhe. Omar.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TWPG, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, amemshukuru Waziri wa Fedha kwa kukubali kuwa mgeni rasmi pamoja na mchango wake katika kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia kupitia sera na mipango ya maendeleo ya taifa.
Amesema semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo wabunge kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika hatua zote za upangaji, utekelezaji na ufuatiliaji wa bajeti, ili kuhakikisha huduma na fursa za maendeleo zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
Katika mafunzo hayo, wabunge walielezwa kuwa sekta za kilimo, afya na maji zimeendelea kuimarisha uwekezaji unaolenga kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake, watoto na makundi maalum, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti jumuishi.
Semina hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha uelewa na ushiriki wa wabunge katika kusimamia bajeti yenye kuzingatia usawa, ujumuishi na maendeleo endelevu kwa wananchi wote.




Comments
Post a Comment