📍Dodoma
Tume ya Madini imeendelea kuimarisha ukaguzi wa migodi nchini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa lengo la kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, hatua inayolenga kuhakikisha rasilimali za madini zinanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza Juni 19, 2026, katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Afisa Mkaguzi wa Migodi wa Tume ya Madini, Rose Mika, amesema ukaguzi wa mara kwa mara unaofanyika katika migodi mikubwa, ya kati na midogo unalenga kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendeshwa kwa kuzingatia Sheria ya Madini pamoja na Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za mwaka 2010.
Amesema ukaguzi huo husaidia kubaini mapema changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama wa wafanyakazi na wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya migodi, hivyo kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kabla ya kutokea kwa madhara.
Rose amesema Tume ya Madini pia inaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa mazingira, ikiwemo kudhibiti uchafuzi wa maji, hewa na ardhi pamoja na kuhakikisha taka zinazotokana na shughuli za uchimbaji zinahifadhiwa na kushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Aidha, amesema Tume inafuatilia utekelezaji wa mipango ya kufunga migodi (Mine Closure Plans) ili kuhakikisha maeneo yaliyokwishafanyiwa uchimbaji yanarejeshwa katika hali salama na yenye tija baada ya shughuli hizo kukamilika.
Kwa mujibu wa Rose, hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha ukuaji wa sekta ya madini unaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Mbali na ukaguzi wa migodi, Tume ya Madini inaendelea kusimamia matumizi ya baruti katika shughuli za uchimbaji, ikiwemo utengenezaji, uingizaji, usafirishaji na biashara yake kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Tume ya Madini inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini pamoja na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kwa kuzingatia matakwa ya sheria, ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.






Comments
Post a Comment