Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni ukumbusho muhimu kwa jamii kuhusu wajibu wa kulinda, kuendeleza na kuhakikisha haki za watoto zinazingatiwa ipasavyo, sambamba na kuenzi mapambano ya watoto wa Soweto waliopigania haki ya kupata elimu bora nchini Afrika Kusini.
Akizungumza Juni 16, 2026 jijini Dodoma, Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka elimu kama kipaumbele kikuu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayesisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania anapaswa kupata elimu bila ubaguzi.
Amesema Serikali imeimarisha jitihada za kuhakikisha usawa na ujumuishi katika sekta ya elimu, hususan kwa watoto wote wakiwemo wasichana, ili kuwawezesha kupata fursa sawa ya kujifunza na kufikia malengo yao ya maisha.
“Hakuna mtoto atakayeachwa nyuma katika mfumo wa elimu.
Hata mabinti waliopata ujauzito wanaruhusiwa na wanapaswa kurejea shuleni kuendelea na masomo yao,” amesisitiza Prof. Mkenda.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya shule ili yawe salama, rafiki na wezeshi kwa wanafunzi wote, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi wa kujifunza na kukuza maendeleo ya kielimu.
Prof. Mkenda ametoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, mashirika na wadau wa maendeleo kuungana na Serikali katika kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu bora, huduma za afya, maji safi na mazingira salama kwa ukuaji na maendeleo yao.



Comments
Post a Comment