Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Ghati Zephania Chomete, ameendelea kushiriki Mkutano wa 19 wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika unaoendelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini, ukiwaleta pamoja viongozi wa mabunge kujadili masuala muhimu yanayogusa maendeleo ya bara la Afrika.
Katika siku ya pili ya mkutano huo, Mwakilishi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Cecilia Paresso, aliwasilisha mada iliyojikita katika nafasi ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola katika kuwawezesha vijana wa Afrika kushiriki kikamilifu katika kufanikisha maendeleo endelevu.
Akiwasilisha mada hiyo, Mhe. Paresso alisisitiza kuwa mabunge yana wajibu mkubwa wa kutunga sheria, kupitisha sera na kuimarisha mifumo inayowapa vijana mazingira rafiki ya kushiriki katika uchumi jumuishi, uongozi na ubunifu. Alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya wakazi wa Afrika ni vijana wenye umri chini ya miaka 30, jambo linaloifanya rasilimali hiyo kuwa nguvu muhimu katika maendeleo ya bara.
Aidha, alieleza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzishwa kwa Wizara inayosimamia masuala ya vijana, upatikanaji wa mikopo, pamoja na utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuwaongezea uwezo wa kiuchumi, ajira na ujasiriamali.
Mkutano huo unawakutanisha Maspika na viongozi wengine wa Mabunge kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola barani Afrika kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo endelevu, utawala bora, na mchango wa Mabunge katika kuimarisha demokrasia na ustawi wa wananchi.


Comments
Post a Comment