ELIMU YA ULINZI NA USALAMA BINAFSI WA MTOTO YATOLEWA KATIKA KAMBI YA WATOTO YA KANISA LA ROC DODOMA.
Katika kuhakikisha Watoto wanakuwa na uangalizi mzuri kuanzia ngazi ya familia Kanisa la ROC Dodoma limewapatia elimu ya ulinzi na usalama binafsi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uwezo wa kujilinda dhidi ya changamoto na vitisho mbalimbali vinavyowakabili katika jamii ya sasa.
Akishiriki katika Mafunzo hayo Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kipolisi Mtumba Mrakibu wa Polisi (ASP)Charles Mwamtobe aliwahimiza watoto kuwa waangalifu na kutambua mapema viashiria vya hatari vinavyoweza kuhatarisha usalama wao, ikiwemo ukatili, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya teknolojia, dawa za kulevya, biashara haramu ya binadamu pamoja na ushawishi wa makundi yenye mienendo isiyofaa.
Alieleza kuwa mtoto si mali ya familia pekee, bali ni tumaini la jamii na taifa la leo, hivyo anapaswa kulindwa na kupewa malezi bora yatakayomwezesha kukua katika mazingira salama, yenye maadili mema na hofu ya Mungu.
“Ulinzi na usalama wa mtoto si jukumu la serikali pekee wala wazazi peke yao, bali ni wajibu wa kila mwanajamii kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kukua na kutimiza ndoto zao,” alisema.
Aidha, washiriki wa kambi hiyo walikumbushwa umuhimu wa kutoa taarifa kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini au vyombo vya dola wanapokutana na vitendo vinavyohatarisha usalama wao au wa wenzao.
Mafunzo hayo yalisisitiza pia matumizi salama ya mitandao ya kijamii na teknolojia ya mawasiliano ili kuwakinga watoto dhidi ya ulaghai, unyanyasaji wa mtandaoni na athari nyingine zinazoweza kujitokeza kupitia matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia.
Kwa upande wake, Kanisa la ROC Dodoma limeendelea kutumia kambi hiyo kama jukwaa la kuwajenga watoto kiroho, kimwili na kijamii, kwa kuwapatia elimu mbalimbali zinazolenga kuwaandaa kuwa raia wema na viongozi bora wa baadaye.
Neno la Mungu katika kitabu cha Mithali 22:6 linasema: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.” Kauli hiyo imeendelea kuwa msingi wa malezi bora yanayolenga kumkuza mtoto katika maadili mema na maisha yenye manufaa kwa jamii.









Comments
Post a Comment