Na Mashaka Mhando, KILINDI
ZAIDI ya wananchi 12,414 wa vijiji vya Nkama, Kwastemba na Kwamwande wilayani Kilindi, wanatarajiwa kuondokana na adha ya maji kufuatia Mradi wa Maji wa Nkama Mnazi unaogharimu Shilingi 853,166,702 kufikia asilimia 75 ya utekelezaji wake.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa matunda ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayotoa kipaumbele kwenye uboreshaji wa huduma za maji safi na salama vijijini na mjini.
Akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Songe, Mhandisi Philipo Bajuta, alisema mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi Sajo Civil Engineering kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji HTM, unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 23, 2026.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mohamed Salim, aliwapongeza watendaji kwa usimamizi mzuri uliowezesha kazi kufika asilimia 75, licha ya kuwepo kwa changamoto ya kuchelewa kwa baadhi ya fedha.
Sambamba na pongezi hizo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tanga, Swaibu Mwanyoka, alionyesha kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo, huku akiishauri Wizara ya Maji kuharakisha utoaji wa fedha zilizosalia ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika haraka.
Mchanganuo wa Fedha na Utekelezaji
Mhandisi Bajuta alieleza kuwa mradi huo ulianza Machi 25, 2025, na ulitarajiwa kukamilika Machi 24, 2026. Hata hivyo, kutokana na kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi katika awamu ya kwanza na ya pili, lilitolewa nyongeza ya muda wa miezi sita.
"Hadi sasa Serikali imeshalipa kiasi cha Shilingi 453,418,742, ambayo ni sawa na asilimia 53.15 ya gharama zote za mradi, huku utekelezaji wa ujenzi ukiwa umefikia asilimia 75," alifafanua Mhandisi Bajuta huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kusimamia miundombinu hiyo.
Hatua za Kiufundi Zilizofikiwa
Akifafanua kazi mbalimbali zinazoendelea site, Mhandisi Bajuta alitaja kuwa ununuzi wa pampu na uunganishaji wa nishati ya umeme umekamilika kwa asilimia 100, na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa mita 14,939 umefikia asilimia 95.
Kazi nyingine ni pamoja na ujenzi wa vituo vinane (8) vya kuchotea maji uliofikia asilimia 80, na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 150,000 uliofikia asilimia 75. Hatua pekee ambayo haijaanza ni ujenzi wa Valve Chamber ambao upo asilimia sifuri.



Comments
Post a Comment