Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Adkin Mwalunenge, anaelezwa kuendelea kuweka msukumo mkubwa katika utekelezaji wa agenda ya maendeleo na mageuzi ya uchumi kwa wananchi wa jimbo hilo kupitia mikakati mbalimbali inayolenga kukuza biashara, uwekezaji, ajira na kuboresha miundombinu ya kiuchumi.
Katika kipindi kifupi tangu achaguliwe kuongoza jimbo hilo, Mwalunenge ameendelea kushirikiana na wananchi kwa kushuka katika maeneo mbalimbali kusikiliza kero zao, kubaini changamoto zinazowakabili na kuzisimamia ili zipatiwe ufumbuzi.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha maendeleo ya jimbo yanakwenda sambamba na mahitaji halisi ya wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ofisi ya Mbunge imejenga mfumo wa kupokea, kuchambua na kufuatilia changamoto za wananchi, huku ikielekeza nguvu katika utekelezaji wa miradi yenye tija kwa uchumi wa Mbeya Mjini na Jiji la Mbeya kwa ujumla.
Miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele ni kukuza biashara za Mbeya ili ziweze kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa, kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kupitia mpango wa Special Economic Zone (SEZ), pamoja na kuandaa mpango wa kuboresha miundombinu ya barabara za jiji kwa kujenga Ring Road na kuunganisha barabara muhimu za biashara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma.
Aidha, mbunge huyo anaelezwa kuweka mkazo katika kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi kwa lengo la kuongeza kipato cha kaya, kukuza biashara ndogo na za kati, pamoja na kuwezesha makundi ya vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo kujikwamua kiuchumi.
Katika juhudi hizo, makundi ya bodaboda, machinga na wajasiriamali yameendelea kupewa kipaumbele kupitia mikakati ya kuyaunganisha na fursa za mikopo na mitaji ili yaweze kukuza biashara zao na kuongeza uwezo wa kujitegemea kiuchumi.Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa jitihada hizo zimeungwa mkono na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Mwalunenge anaelezwa kuwa amekuwa akifanya kazi kwa karibu na wananchi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha mipango ya maendeleo ya Jimbo la Mbeya Mjini inatekelezwa kwa ufanisi, huku akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pale ambapo wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika kupanga na kutekeleza miradi inayowagusa moja kwa moja.
Dhamira ya Mbunge Patrick Mwalunenge ni kuifanya Mbeya Mjini kuwa kitovu cha biashara, uwekezaji na uzalishaji kitakachochochea ukuaji wa uchumi wa jiji na kuongeza ustawi wa wananchi kupitia maendeleo jumuishi na endelevu.



Comments
Post a Comment