Wananchi wa Kata ya Zuzu, Jijini Dodoma, wameibuka na malalamiko makali yenye hisia nzito na machungu makubwa, wakimlenga Diwani wa kata hiyo kwa kumtuhumu kuhusika katika kufungwa kwa eneo la uchimbaji wa kokoto na mchanga ambalo lilikuwa mkombozi wao wa maisha kwa zaidi ya wananchi 300.
Kwa sauti zilizotawaliwa na huzuni, hasira na wakati mwingine machozi yakibubujika, wananchi hao wamesimulia jinsi maisha yao yalivyoporomoka ghafla kufuatia kufungwa kwa eneo hilo, wakisema walikuwa wakitegemea uchimbaji huo kama chanzo kikuu cha kipato cha kila siku.
Wamesema kupitia shughuli hizo walikuwa wakigharamia mahitaji ya familia, ada za shule za watoto na matumizi ya msingi ya nyumbani, lakini sasa wamebaki wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha isiyo na uhakika wala matumaini.
Kwa hisia kali na maumivu ya wazi, wananchi hao wamedai kuwa uamuzi wa kufungwa kwa eneo hilo ulifanyika bila kushirikishwa wala kufanyika mkutano wa pamoja wa wananchi, jambo ambalo wamesema limeongeza hasira, maumivu na sintofahamu ndani ya jamii.
Aidha, wamedai kuwa Diwani hakuhudhuria mikutano mitatu iliyowahi kuitishwa kwa lengo la kutaka ufafanuzi, hali waliyosema imezidisha mgogoro na kuwafanya wananchi kujiona hawasikilizwi na viongozi wao.
Katika tuhuma zao zilizojaa hisia kali, wananchi hao wanahisi huenda kuwepo kwa maslahi binafsi nyuma ya uamuzi huo, wakidai kuwa kuna eneo jingine la uchimbaji lililopo kata hiyo ambalo chimbo hilo anahusika nalo diwani Kwa maslahi yake binafsi.
Wamesema eneo lililofungwa lilikuwa na neema ya malighafi iliyowawezesha kujipatia kipato cha kila siku bila shida, tofauti na eneo mbadala ambalo wamelielezea kuwa halina uzalishaji wa kuridhisha.
Kwa sauti zinazoonyesha uchungu mkubwa na kukata tamaa, wananchi hao wamemtaka Diwani huyo kujitokeza mbele yao hadharani kutoa ufafanuzi wa kina, wakisema ukimya wake unazidi kuchochea hasira na kupoteza imani kwa uongozi.
Baada ya wananchi kuzungumza na waandishi wa habari, walimpigia simu Diwani wa Kata ya Zuzu, Mhe. Jenesta Malingo, ambapo alijibu kwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) akisema: “Tatizo kuna baadhi ya watu yawezekana wana maslahi yao binafsi wanashawishi baadhi ya wananchi kutoheshimu mamlaka hizo.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mazengo, Joshua William Kajembe, amesema hatua ya kufungwa kwa eneo hilo imewaumiza sana wananchi zaidi ya 300 waliokuwa wakitegemea uchimbaji huo kama chanzo kikuu cha maisha yao, akisisitiza kuwa jamii sasa inahitaji suluhisho la haraka.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Zuzu, Omary Bilali, ameeleza kusikitishwa na diwani kutohudhuria mikutano iliyomualika kwa ajili ya kutoa ufafanuzi, akisema hali hiyo imeongeza mpasuko, hasira na sintofahamu miongoni mwa wananchi na kuathiri imani ya uongozi wa chama na serikali ya kata hiyo.











Comments
Post a Comment