Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Wizara ya Fedha, Benki Kuu na taasisi za fedha nchini kuimarisha mazingira ya upatikanaji wa mikopo, kupunguza gharama za mikopo na kuongeza ushindani ili kunufaisha sekta binafsi, wanawake, vijana, wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Ametoa agizo hilo leo katika hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania, yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. Samia amesema mafanikio ya mfumo wa fedha hayapaswi kupimwa kwa idadi ya wananchi waliofikiwa na huduma za kifedha pekee, bali kwa matokeo yake katika kipato, biashara, ajira na ustawi wa wananchi wenyewe.
"Kipimo chetu kisiwe tu idadi ya wananchi waliofikiwa na huduma za fedha, bali namna huduma hizo zilivyowaongezea kipato, kupanua biashara, kuwawezesha wakulima kupata mitaji kwa wakati, kuwasaidia vijana kuanzisha kampuni, na kujenga akiba za familia," amesema Rais Dkt. Samia.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa taasisi za fedha nchini kupitia upya riba, ada, bima, masharti ya dhamana na muda wa marejesho ya mikopo, ili kuongeza upatikanaji wa mikopo yenye gharama nafuu kwa wananchi wengi zaidi.
Vilevile, ametoa wito kwa taasisi za fedha nchini kupitia upya vigezo vyao vya tathmini ya utoaji mikopo, kwa kuzingatia historia ya biashara, mauzo na mwenendo wa malipo kwa waombaji, badala ya kutegemea dhamana za jadi pekee, hasa kwa wanawake, vijana, wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunahitaji mageuzi katika sekta ya fedha yanayokwenda zaidi ya mfumo uliopo wa kiutendaji ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya uchumi, teknolojia na masoko ya fedha.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Benki Kuu katika kuimarisha sera, usimamizi wa sekta ya fedha na mazingira ya uwekezaji, ili mfumo wa fedha uchochee zaidi uzalishaji, biashara na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Naye, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema Benki Kuu imeendelea kulinda utulivu wa bei, kusimamia sekta ya fedha, kuimarisha mifumo ya malipo na kuongeza huduma jumuishi za kifedha nchini.
Amesema mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kutoka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa mwaka 1994 hadi takriban asilimia 16 mwaka 2025, huku mikopo chechefu ikishuka hadi asilimia 2.9 mwezi Februari, 2026, wakati akiba ya fedha za kigeni ikitosheleza manunuzi na huduma katika kipindi cha zaidi ya miezi minne.
"Benki Kuu (ya Tanzania) ya leo ni miongoni mwa benki kuu zinazoongoza Afrika katika kusukuma huduma jumuishi za kifedha," amesema Dkt. Hannig, na kuongeza kuwa Tanzania imejenga nafasi ya kipekee katika historia ya AFI kupitia uongozi wake, ubunifu wa kidijitali, mifumo ya malipo ya papo kwa papo na kanuni zinazolinda watumiaji wa huduma za fedha.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia ametunukiwa Tuzo Maalumu ya "Kinara wa Mageuzi ya Mifumo na Huduma Jumuishi za Kifedha" inayotambua mchango wake katika kuendeleza mageuzi ya huduma za kifedha nchini.





Comments
Post a Comment