Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

MWANAFA AFUNGA UMITASHUMTA, AELEZA MKAKATI WA SERIKALI


📍 Bilioni 15 kukamilisha ujenzi akademia ya michezo Malya

NA Mashaka Mhando, Iringa

SERIKALI imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 15 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Akademia ya Taifa ya Michezo iliyopo Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

Hatua hiyo ya kiserikali inalenga kuweka mfumo thabiti na wa kudumu wa kuibua, kulelea, na kukuza vipaji vinavyopatikana kupitia mashindano ya shule za msingi na sekondari (UMITASHUMTA na UMISSETA).

Hayo yamebainishwa jana, Juni 17, 2026, na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), wakati akifunga rasmi mashindano ya UMITASHUMTA yaliyokuwa yakifanyika mkoani Iringa.











Mhe. Mwinjuma alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza kwa nguvu kubwa katika sekta ya michezo na sanaa, ikitambua mchango wake katika kuzalisha ajira, kujenga afya, na kuongeza ushindani wa Taifa kimataifa.

Malya Academy na Matunda ya Serengeti Boys

Akifafanua kuhusu matumizi ya Akademia hiyo ya Malya, Mhe. Mwinjuma alisema kituo hicho kitakuwa na uwezo mkubwa wa kupokea na kuendeleza vipaji vinavyogunduliwa kwenye mashindano ya shule, ili kuandaa kizazi cha dhahabu kitakachowakilisha Taifa.

Kuthibitisha ubora wa mashindano hayo, Naibu Waziri aliweka wazi matokeo chanya yaliyoonekana hivi karibuni kupitia Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys). 

"Mafanikio ya Serengeti Boys yameonyesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza kwenye michezo ya shule. Wachezaji wasiopungua watano wa kikosi hicho, akiwemo golikipa namba moja, ni zao halisi lililotokana na mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA," alibainisha Mhe. Mwinjuma.

Maandalizi ya FEASSSA Morogoro

Aidha, Mhe. Mwinjuma alihitimisha kwa kueleza kuwa mashindano yaliyofungwa Iringa ni msingi muhimu wa kuandaa wawakilishi wa Tanzania watakaoshiriki Mashindano ya Michezo ya Shule kwa Nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA).

Mashindano hayo makubwa ya kikanda yanatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu mkoani Morogoro, ambapo Naibu Waziri amewataka wanamichezo wote waliochaguliwa kuunda timu ya Taifa kambi kufanya maandalizi kabambe ili kuitangaza vyema Tanzania na kubakiza makombe nyumbani

Comments